Meneja wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Pep Guardiola amewatisha wapinzani wake kwa kuwaambia Mshambuliaji Erling Haaland anaendelea alipoishia na sasa anaonekana kuwa fiti zaidi, hivyo ni ujumbe unaopaswa kuzingatiwa na mabeki wote kwa msimu ujao.
Guardiola amekoshwa na kiwango cha mshambuliaji wake huyo baada ya kufunga mara mbili wakati Manchester City ilipoichapa Yokohama Marinos ya Japan mabao 5-3 katika mchezo wa kirafiki wa kipindi hiki cha kujiandaa na msimu mpya wa 2023-24.
Haaland, ambaye alifunga mabao 52 wakati Man City iliposhinda mataji matatu kwenye msimu wake wa kwanza huko Etihad, ameanza kwa moto baada ya kutokea benchi dhidi ya Yokohama Marinos na kutikisa nyavu mara mbili.
Mtambo huo wa mabao wa Etihad ulihitaji dakika sita tu za kuwa ndani ya uwanja kufunga bao na alihitaji kugusa mipira mitatu tu kabla ya kuusukumia nyavuni na kuisaidia Man City kuibuka na ushindi baada ya mabao ya kusawazisha kutoka kwa John Stones na Julian Alvarez.
Na baada ya mechi, Guardiola alisema: “Ukilinganisha na muda kama huu wa sasa yupo fiti zaidi kuliko vile msimu uliopita, Erling alivyotua. Yupo vizuri. Bado hajafikia kwenye ubora wake, lakini kwake jambo muhimu ni kufunga.”
Haaland alifunga bao moja tu katika mechi nane za mwisho za Man City kwa msimu uliopita.
Lakini, sasa ameanza kwa moto kwenye kipindi hiki majira ya kiangazi kwenye mechi za maandalizi ya msimu mpya.