Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pengine Job ni mzalendo kuliko Morocco

Job X Morocco Shida Pengine Job ni mzalendo kuliko Morocco

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baadhi tumeshikwa na butwaa tangu kaimu kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ aeleze sababu za kumuacha beki mahiri wa Yanga, Dickson Job kwenye kikosi chake kinachokwenda kucheza mechi mbili za mashindano maalum ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) yaliyobatizwa jina la Fifa Series.

Pamoja na kwamba beki huyo wa kimataifa wa Yanga hakupangwa hata mechi moja ya fainali zilizopita za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 Ivory Coast, haikutegemewa angeachwa na makocha wa Stars katika kipindi hiki ambacho beki huyo ameshiriki kuivusha klabu yake hadi robo fainali za Ligi ya Mabingwa wa Afrika, tena baada ya kupata ushindi mkubwa mbele ya CR Belouizdad ya Algeria, moja ya mataifa yanayosumbua katika soka barani Afrika.

Lakini baada ya kikosi kutangazwa bila ya Job kuwepo ndipo mjadala mkubwa ulipoibuka na baadaye habari kusambaa kwamba eti alikataa kupangwa kama beki wa kulia wakati wa fainali za Afcon huko Ivory Coast.

Mbali na kusema hayo, kocha Morocco alisema Job alionyesha kutokuwa mzalendo kwa kukataa kucheza nafasi ambayo hajaizoea, licha ya kocha wa Yanga kuanza kumchezesha katika siku za hivi karibuni kunapokuwa na tatizo la majeruhi au uchovu na hivyo kulazimika kupumzisha baadhi ya wachezaji.

Kama ambavyo wengi wamekuwa wakituhumu kwamba makocha wamekuwa wakipelekwa puta na hoja za wachambuzi, Morocco aliangukia hukohuko katika mpango wake wa kutomtumia Job kama beki wa kati. Alisema Job hawezi kucheza kama beki wa kati kwenye kikosi chake, eti kwa sababu ni mfupi, hoja ambayo imekuwa ikitumiwa na wachambuzi wengi kumkosoa beki huyo aliyetokea timu za vijana.

Ni hoja ambayo haina utetezi wowote wa maana licha ya makocha wengi kupenda kutumia wachezaji warefu kwenye nafasi za kati katika ulinzi na katika ushambuliaji.

Tukisema tumtajie mabeki wafupi duniani, itakuwa ni kama kudhihirisha kuwa Morocco hakuwa na hoja zozote zaidi ya kuingia kwenye mfumo wa wachambuzi wa kupinga uwezo wake kwa kutumia kimo.

Lakini beki aliyeondokea kuwa mmoja wa mabeki maarufu duniani, ni Carles Puyol, ambaye enzi zake za mwanzo katika soka alianzia kama beki wa kulia, lakini uwezo wake mkubwa wa kuongoza ngome ulimfanya ahamishwe na kuwa beki wa kati wa klabu kubwa ya Barcelona, akiiongoza kutwaa mataji yote yaliyokuwa mbele yake, hali kadhalika nchi yake ambayo wastani wa kimo kwa mabeki ni 5’10.

Bila shaka Fabio Canavaro (5’9) hawezi kukosa kwenye orodha hiyo ya mabeki wafupi, akiwa ameiongoza Italia kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2006 na ndiye beki pekee hadi sasa kushinda tuzo ya Ballon d’Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia. Kutokana na ufupi wake kocha alikuwa akimpanga na Marco Materrazi ambaye ni mrefu na ambaye alijua kucheza na mabeki wafupi wa kati.

Orodha ni ndefu na yenye majina makubwa, lakini ukitaja majina ya wachezaji wa barani Ulaya, utaambiwa usijilinganishe nao kana kwamba huko wanacheza bao.

Lakini George Masatu ni mfano mwingine wa mabeki wafupi wa kati ambaye aliiongoza Simba kwa mafanikio mwishoni mwa miaka ya tisini. Na Yanga pia waliwahi kuwa naye Paul John Masanja, mmoja wa wachezaji walioiwezesha Yanga kuwa timu ya kwanza kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Ingawa mabeki wa kati wafupi ni wachache, hakuna sababu za kisayansi zinazotolewa kuhalalisha wasicheze kati.

Beki maarufu wa zamani wa Italia na ambaye pia ni mfupi, Franco Baresi alisema: “Ninapoona nalazimika kulala ili kuufikia mpira kwa mguu, natambua kuwa kuna kosa nimefanya.”

Alisema hayo kumaanisha kuwa hoja si ufupi bali ni uwezo wa kuusoma mchezo wakati mpira ukichakatwa kuelekea langoni na kujua nini ufanye kabla ya kulazimika kupiga ngwala.

Ndivyo alivyo Dickson Job ambaye huweza kucheza mipira ya juu mbele ya mabeki warefu na hunasa sana pasi zinazoelekea golini kwake na kwa nadra huonekana kulala kuufuata mpira kwa mguu wake kumaanisha kuwa hakukuwepo na njia nyingine ya kulinusuru lango lake.

Nilitegemea kuwa Morocco, kwa kuwa aliamua kutoka hadharani kuzungumzia sababu za kumuacha Job, angewaambia waandishi jinsi beki huyo alivyoiathiri Stars kila alipopangwa kama beki wa kati, kiasi cha kuamua kutomteua safari hii.

Kwamba katika mechi fulani alishindwa kuufuata mpira wa juu kwa sababu mshambuliaji alikuwa mrefu zaidi yake, au alipopiga ngwala mguu wake haukuweza kuufikia mpira na hivyo kumpa nafasi mshambuliaji kufunga au kusababisha penalti.

Lakini mara nyingi makocha wenye maadili huwa hawapendi kuzungumzia wachezaji waliowaacha kwa kuwa wako wengi kuliko aliowateua. Hii ni kanuni kubwa na muhimu kwa sababu humuepusha kocha kusema mambo ambayo yatamshtaki baadaye.

Lakini kitu alichovuruga kabisa kocha huyo ni hoja kwamba eti Dickson Job hana uzalendo! Hana uzalendo kwa kukataa kucheza nafasi ambayo hajaizoea? Alitaka Job apuyange tu na makosa yoyote yawe juu yake na si athari ambazo timu ingepata? Nani ni mzalendo kati ya wawili hao?

Ninachofahamu, kabla ya mechi makocha huamua kuzungumza ana kwa ana na wachezaji, hasa wale ambao anawabadilishia majukumu ili aone utayari wao. Na hii hufanyika kwa kocha kuzungumza na mchezaji akiwa amemkazia macho ili asome hisia zake kama zinalingana na anachosema.

Kwangu, katika mazingira hayo, mchezaji ambaye atasema hawezi jukumu ninalompa, basi huyo atakuwa amerahisisha kazi kuliko kumlazimisha kucheza ukijua kabisa mchezaji amesema hawezi kuimudu nafasi au majukumu uliyompa.

Anayekataa jukumu alilobadilishiwa, huyo ndiye mzalendo kwa kuwa amesema kile ambacho anakiamini kuliko yule ambaye angekubali huku moyoni akijua kuwa hawezi.

Hata kama kwenye klabu yake huchezeshwa kama beki wa kulia katika baadhi ya mechi, hayo hutegemea na majukumu ambayo mwalimu anampa kulingana na ugumu wa mechi na usaidizi ambao angeupata. Mechi dhidi ya Algeria, Job alicheza kama beki wa kulia, lakini msaidizi wake wa karibu alikuwa Haji Mnoga, ambaye hakuna mwenye shaka naye kuhusu uwezo wake wa kuzuia.

Hivyo, mchezaji aliyekataa jukumu ambalo hajalizoea, hasa anapoitumikia timu ya taifa, huyo ni mzalendo kuliko yule anayemlazimisha kucheza nafasi ambayo anajua kabisa kuwa mchezaji hajaizoea na hivyo ni kubahatisha kumpanga.

Na kama Job angekubali na baadaye kufanya makosa ambayo yangeigharimu timu, ni dhahiri kuwa wengi wangesahau athari za Stars kupoteza mchezo na wangejikita zaidi kujadili makosa ya beki. Hapo nani angekuwa mzalendo?

Ni muhimu kwa makocha kuacha tabia hii inayozidi kukua ya kutangaza matatizo ya wachezaji na kuwashushia lawama kwa matokeo ambayo hayakuwa mazuri. Ni dhahiri kwamba mashabiki wakichanganua sana wataona sababu za Stars kutovuka hatua ya makundi ni pamoja na Job kukataa kucheza kama beki wa kulia.

Wakati mwingine tunapotangaza kasoro za wachezaji, tunaonyesha udhaifu wetu kimaadili na kitaaluma. Na hapa, Morocco ameonyesha kuwa alikosa uzalendo kuliko Job ambaye aliona angeliangusha taifa kwa kucheza nafasi ambayo anaamini haimudu vizuri.

Chanzo: Mwanaspoti