Mwanasiasa wa Nigeria Dkt. Cairo Ojougboh ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha All Progressives Congress amefariki Dunia juzi Jumatano jioni alipokuwa akitazama mechi ya nusu fainali ya kombe la Mataifa Afrika 2023 (AFCON 2023) kati ya Nigeria na Afrika Kusini.
Chanzo cha karibu na mwanasiasa huyo kimesema, “Cairo Ojougboh, daktari alifariki wakati wa mechi ya Nigeria dhidi ya Afrika Kusini.
“Tukio hilo lilitokea wakati Afrika Kusini walipopewa penalti dhidi ya Nigeria muda mfupi baada Nigeria kuonekana kufunga bao la pili ambalo lilikataliwa.”
“Inaelezwa Dkt. Ojougboh alipiga kelele na kuanguka kutokana na mshtuko mkubwa wa moyo wakati Afrika Kusini ilipofunga bao.”
Victor Osimhen aliifungia Nigeria bao la pili kabla ya VAR kubatilisha bao hilo na kuizawadia Afrika Kusini penalti kufuatia uchunguzi wa madhambi yaliyofanyika sekunde chache kabla ya bao hilo.
Hata hivyo ‘The Super Eagles’ walifanikiwa kufuzu kwenye fainali kwa ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Afrika Kusini.