Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Penalti hazikutakiwa fainali Ngao ya Jamii

Ally Salim Ngaoo Wachezaji wa Simba wakiwa wamembeba Ally Salim baada ya kuokoa mikwaju ya Penati

Wed, 16 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bado mpira wetu una shida kubwa ya waamuzi. Bado mpira huo una shida kubwa ya washambuliaji. Bado mpira una shida kubwa ya mashabiki.

Kama waamuzi wangekuwa makini, pengine Simba wasingefika fainali. Shughuli yao ingeishia mikononi mwa Singida Fountain Gate.

Kama waamuzi wangekuwa makini huenda tusingefika dakika 90 kwenye mechi ya fainali. Faulo ya Khalid Aucho wa Yanga dhidi ya Kibu Dennis wa Simba ingeipa Simba penalti na huenda shughuli ingeishia hapo.

Bado tuna shida kubwa ya waamuzi. Kama waamuzi wangekuwa vizuri huenda fainali ya Ngao ya Jamii ingekuwa ni Singida Fountain Gate dhidi ya Yanga. Ndiyo mpira wetu ulivyo kama waamuzi wangekuwa makini, huenda bao la Yanga lililokataliwa juzi kwa madai kuwa Clement Mzize ameotea lingesimama na Yanga ingepata bao la kuongoza. Hakukuwa na kuotea (off side) yoyote na Yanga ilinyimwa bao halali.

Mpira wetu kuna wakati ukiwa mbali unaona kama umepiga hatua kubwa mbele kumbe ukiwa kwa karibu unagundua pia kumbe tuna hatua nyingine nyingi tu za kurudi nyuma.

Hongereni sana Simba kwa ubingwa, lakini hamkustahili hata kufika tu fainali. Hongereni Yanga kwa kufika hatua ya penalti, lakini Kibu Dennis alitakiwa kupewa penalti kwa madhambi ya Aucho.

Hata kama kusema kila siku haisaidii hatuwezi kusema kwa sababu ndiyo njia bora zaidi ya kutatua changamoto. Waamuzi pia ni binadamu, lakini hawa wa kwetu kiboko. Moja ya fainali zenye waamuzi wabovu ni hii ya FA Tanga. Ni kama walikuwa na ajenda binafsi. Tumepata mechi ya fainali ambayo haikustahili. Tumepata bingwa tena ambaye hakustahili.

Pamoja na huo upungufu wote Simba ndiyo bingwa wa Ngao ya Jamii 2023. Hii haijalishi unapenda au hupendi. Simba ndiyo bingwa. Wakati Simba inawatambulisha kina Willy Onana, Aubin Kramo, Luis Miquissone na wengine wengi ililenga kuwa kwenda kuiona Simba ya moto kwelikweli.

Baada ya Kambi ya Uturuki na mechi ya Simba Day wasiwasi ukaanza kutanda. Baada ya kucheza mechi ya kwanza ya Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate wasiwasi ukazidi. Baada ya mechi dhidi ya Yanga, Simba imeshinda lakini Simba hawana raha. Unajua kwa nini?

Ni rahisi tu. Wana Simba wengi hawakuona kile walichotarajia. Simba inashinda, lakini mashabiki hawana furaha. Hawana imani na timu yao. Imeshinda kwa kudra za Mungu na sio ubora unaoonekana. Kama waamuzi wangechezesha kwa haki, Simba isingechomoka mechi ya Singida Fountain Gate. Kama waamuzi wangechezesha vizuri, Mnyama angekufa mapema tu.

Yanga wanaonekana kuwa na timu nzuri, lakini nao bado hawana mshambuliaji wa uhakika. Mzimu wa Fiston Mayele bado unawaandama. Mechi kama ile ya fainali wangekuwa na Mayele, Mnyama angekufa mapema tu.

Clement Mzize ni mchezaji mzuri, lakini bado anaendelea kujifunza. Mechi za fainali sio za kitoto. Ni mechi za kikubwa zinazohitaji wachezaji wakubwa. Kama nafasi walizopata Yanga zingetumika sawasawa tusingefika hatua ya penalti.

Kumekuwa na kelele nyingi za Yanga kulalamika juu ya kipa wa Simba, Ally Salim kuwa alikuwa anatoka hatua moja mbele kabla ya mpira kupigwa wakati wa penalti. Ni kweli. Ni kosa kikanuni kufanya hivyo.

Kimsingi penalti tatu kati ya nne zilipaswa kurudiwa. Pamoja na haya yote turudi palepale kuwa Yanga pia ilikosa wapigaji wazuri. Aziz KI alifunga licha ya kipa kutoka langoni kimakosa. Bado Yanga hawakuwa na wapigaji wazuri.

Mtu anayeweza kumhamisha upande kipa asingelalamikia kipa kutoka mapema. Upigaji mbovu wa penalti za Yanga ndiyo sababu kubwa ya Wananchi kukosa ubingwa. Tatizo la Yanga naona kama wanajiamini sana. Wanaona ni kama Simba na timu nyingine haziwezi kuwafanya kitu.

Kama Yanga wangekuwa na umakini mkubwa pale Mkwakwani tusingefika kwenye hatua za mikwaju ya penalti. Moja kati ya maeneo ambayo Simba na Yanga wana ubora unaokaribiana ni idara zao za ulinzi. Yao Kouassi ni mtu kwelikweli ule upande wa kulia. Lomalisa ni kama amezaliwa upya. Yanga haikamatiki.

Mohammed Hussein na Shomary Kapombe wembe ni uleule. Simba iko mikono salama. Katika mechi zote mbili hakuna timu kati yao iliyoruhusu hata bao moja ndani ya dakika 90. Shida kubwa ya hizi timu ni ubutu kwenye idara ya ushambuliaji. Simba wanajitafuta na hawajajipata. Yanga kwenye ushambuliaji majanga matupu. Hakuna mtu wa uhakika hadi sasa.

Kama timu zote mbili zingekuwa na washambuliaji wa maana tusingefika hatua ya penalti. Mtu angekufa asubuhi tu. Clatous Chama ni mchezaji mzuri akiwa Benjamin Mkapa tu. Ni mara chache sana Chama amewahi kuwa msaada kwa Simba ugenini. Ni mara chache sana huwa anafanya unyama Dar.

Miquissone bado anacheza na kitambi. Angepunguza mwili kidogo. Amekuwa Chibonge. Kutocheza mara kwa mara akiwa Misri nadhani kumechangia jambo hili. Bado anaonekana ana kitu, lakini itachukua muda kumuona amerudi kwenye ubora wake.

Kama John Bocco, Miquissone, Chama wangekuwa fiti tusingefika hatua ya mikwaju ya penalti. Wachezaji wetu wa kigeni wakati mwingine tunawapamba sana wakati tukiwaona uwanjani ni kawaida sana. Ukitazama kwa pande zote mbili utagundua kuwa wachezaji wengi wapya hawana nafasi ya moja kwa moja kwenye vikosi vya kwanza.

Pale Yanga ni Maxi Nzengeli na Yao ndio watu wa uhakika. Pale Simba ni Che Malone na Fabrice Ngoma. Wageni wengi bado wanajitafuta. Wageni wengi bado hawajaaminika kuingia kwenye timu. Pamoja na changamoto zote hongera sana Mnyama kwa ubingwa ingawa mashabiki wako bado wamejawa mashaka.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: