Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pele alipotoa asisti kwa Puma kuifunga bao Adidas

WhatsApp Image 2023 01 04 At 10.jpeg Pele alipotoa asisti kwa Puma kuifunga bao Adidas

Wed, 4 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

ADIDAS na Puma ni kampuni za vifaa vya michezo kutoka Ujerumani.

Hizi ni kampuni mbili zilizotoka kwenye familia moja ya Dassler ambayo ilianza biashara hii miaka ya 1920.

Ndugu wawili wa familia hii, Adolf na Rudolf, walianzisha kampuni yao ya viatu waliyoiita Geda.

Kampuni yao ilipata umaarufu kwenye michezo ya Olimpiki iliuofanyika Berlin, mwaka 1936 baada ya mkimbiaji mweusi wa Marekani, Jesse Owens kuvaa viatu vyao na kushinda medali ya dhahabu.

Miaka ya 1940 ukatokea mgogoro baina ya ndugu hawa wawili uliozaa chuki kubwa baina yao na kufika mwaka 1948 kampuni yao ikaanguka, na kila mmoja akaenda kuanzisha kampuni yake, mmoja akaanzisha Adidas na mwingine akaanzisha Puma.

PUMA

Hii ilianzishwa na Rudolf mwaka 1948 na ilianza kwa jina la Ruda ambalo ni kifupisho cha jina lake la Rudolf. Baadaye ndiyo akaibadilisha na kuiita Puma, alichukua jina la yule mnyama.

ADIDAS

Hii ilianzishwa na Adolf mwaka 1949. Adi ni kifupisho cha jina lake la Adolf, na Das ni kifupisho cha jina la baba yake la Dassler.

Hiki kilikuwa kipindi cha baada ya vita vya pili vya dunia na Ujerumani ilitengwa na jumuiya ya kimataifa ikiwemo michezo.

Hii ilifanya hata bidhaa za nchi hiyo kukosa umaarufu kimataifa.

Ujerumani yenyewe iligawanywa sehemu mbili, Magharibi na Mashariki, kama adhabu ya kuchokoza vita.

Ujerumani Magharibi ikaruhusiwa kushiriki Kombe la Dunia 1954, ambalo ndiyo la kwanza kuoneshwa kwenye TV.

Adidas na Puma yakatumia fursa hii kujitambulisha duniani.

Kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumani Magharibi, Sepp Herberger alikuwa na mgogoro na Rudolf hivyo Puma ikakosa dili la kuidhamini timu hiyo ya taifa. Adidas ya Adolf ikatumia nafasi.

Timu hiyo ikashinda ubingwa na kuifanya Adidas kuwa maarufu sana. Hali hii iliitesa sana Puma, nayo ikatafuta pa kutokea.

Mwaka 1970 ikafanikiwa kumpata Pele, mwanadamu maarufu kuliko wote duniani wakati huo.

Kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Peru, Pele alimuomba mwamuzi asianzishe mpira ili afunge kamba za viatu vyake.

Mwamuzi akakubali na Pele akainama kwa takribani dakika nzima.

Kamera zinaenda hadi miguuni na watazamaji nyumbani wakaona Pele amevaa Puma.

Hili lilikuwa bao la ushindi kwa Puma na kuifunika kabisa Adidas.

Mauzo ya Puma yakapaa maradufu kuizidi Adidas.

Rudolf alifariki mwaka 1974 na Adolf akafariki mwaka 1978.

Chanzo: Mwanaspoti