Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pazia la EPL 2023/2024 kufungwa leo, kila mechi ni muhimu

Skysports Premier League Feature 6211072 Pazia la EPL 2023/2024 kufungwa leo, kila mechi ni muhimu

Sun, 19 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu England fainali ni leo, Jumapili. Mbio za ubingwa. Tiketi ya kucheza Ulaya. Vita ya kukwepa kushuka daraja. Tuzo kwa wachezaji binasi. Kila kitu kitafahamika leo.

Leo ni siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu England 2023-2024. Kuna mambo kibao yatafahamika hatima yake kwenye mechi zitakazochezwa leo, ambapo viwanja 10 tofauti vitawaka moto kwa muda mrefu, kila timu ikijaribu kupambania inachokipambania.

Kwa kifupi, katika siku hii ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu England kila mechi ni muhimu, huku umuhimu mwingine ni kwa wachezaji wanaowania tuzo binafsi, ikiwamo Kiatu cha Dhahabu na ile ya mchezeshaji.

Mambo yanaanzia kwenye vita ya ubingwa, ambapo kila kitu kitafahamika leo kama taji hilo litakwenda Emirates au Etihad, ambapo itakuwa kwa mara ya nne mfululizo. Arsenal na pointi zao 86, watashuka uwanjani Emirates kukipiga na Everton, wakati Man City yenye pointi 88, itakuwa nyumbani pia huko Etihad kukabiliana na West Ham United. Mechi zote hizo ni muhimu, huku kila upande ukiomba mabaya kwa mwenzake, ateleze mambo yaende sawa, endapo yeye atashinda mechi yake. Kwa Arsenal kuchukua ubingwa, kwanza italazimika kushinda mechi yake, huku akiomba Man City iangushe pointi kwa West Ham.

Itawezekana? Jibu la hilo litapatikana leo hii.

Kwenye tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, timu za Ligi ya Mabingwa Ulaya zimeshaweka kibindoni tiketi zao, ambazo ni Man City, Arsenal, Liverpool na Aston Villa baada ya kumaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi. Lakini, kuna nafasi nyingine za kucheza Ulaya, hasa kwenye michuano ya UEFA Europa League na Europa Conference League, ambapo timu zitakazokamatia tiketi hizo, zitafahamika baada ya mechi za leo. Chelsea na Tottenham Hotspur zinagombania nafasi ya tano kwenye msimamo, ili kufuzu mikikimikiki ya Europa League. Chelsea itacheza na Bournemouth, wakati Spurs itakuwa na kibarua na Sheffield United. Kwa Spurs na Chelsea, zenyewe kuwa salama katika nafasi zao, zinahitahi kupata ushindi. Newcastle United na Manchester United, zenyewe zipo kwenye vita ya kuwania tiketi ya kucheza Europa Conference League. Newcastle United itacheza na Brentford, wakati Man United itacheza na Brighton. Vita yao ni ya kugombea nafasi ya saba, ambayo ndiyo inayotoa tiketi ya kucheza michuano hiyo ya Conference League.

Hata hivyo, Man United inaweza kufuzu Europa League kupitia tiketi ya ubingwa wa Kombe la FA, endapo kama itafanikiwa kuifunga Man City katika mchezo wa fainali utakaopigwa Mei 25 huko, Wembley.

Kama Man United itashinda Kombe la FA, basi timu itakayokuwa imemaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, haitacheza Europa League, basi itahamia kwenye michuano ya Conference League.

Na hali ilivyo, timu moja kati ya Spurs, Chelsea na Newcastle inaweza kumaliza kwenye nafasi ya sita.

Ushindi wa Newcastle na kipigo kwa Chelsea kinaweza kuifanya miamba hiyo ya St James' Park kushika nafasi ya sita. Man United kwenye nafasi ya nane, inaweza kufikia pointi 60 za Chelsea endapo itaichapa Brighton na The Blues ikapoteza. Lakini, shida ni tofauti ya mabao ya Man United ina -3 na Chelsea yenyewe ina +13.

Kwenye kushuka daraja, inayotafutwa ni timu ya tatu iliyobaki kwenye kushuka daraja. Luton Town inashika nafasi ya 18 kwenye msimamo na itakipiga na Fulham kutambua hatima yao kama itashuka daraja au itabaki. Kwenye nafasi hiyo, wapo pointi tatu nyuma ya Nottingham Forest, ambao wanaweza kuponyeka kwa kufungwa mabao machache. Forest ina -19 na Luton ina -31. Forest itacheza na Burnley.

Timu mbili ambazo zimeshashuka daraja ni Sheffield United na Burnley. Na bila shaka, Luton ataungana nao, kwa sababu itahitaji kushinda kwa idadi isiyopunguza mabao 12, huku ikiomba Forest ipoteze.

Kwenye vita ya Kiatu cha Dhahabu ni muujiza tu ndiyo utamzuia Erling Haaland asibebe tuzo hiyo baada ya kufunga mabao 27, matano zaidi ya mchezaji anayemfuatia kwenye orodha ya vinara wa mabao. Cole Palmer mwenye mabao 22, atahitaji kufunga zaidi ya mara tano, huku akiomba Haaland asifunge ili kunasa tuzo hiyo, huku vita ikiwa nzito kwa mastaa wengine kama Alexander Isak, mwenye mabao 20 na Dominic Solanke na Ollie Watkins waliofunga mara 19 kila mmoja.

Katika mchakamchaka wa tuzo ya Playmaker, kwa hali ilivyo kwa sasa, Watkins yupo pazuri akiwa ameasisti mara 13 na kuonekana kama ataondoka na tuzo hiyo. Lakini, nyuma yake kuna mastaa saba, walioasisti mara 10 kila mmoja, akiwamo Kevin De Bruyne, ambapo muda wowote mambo yanaweza kubadilika. Wengine wanaosaka tuzo hiyo ni Morgan Gibbs-White, Anthony Gordon, Pascal Gross, Palmer, Mohamed Salah na Kieran Trippier. Mastaa hao, kila mmoja ameasisti mara 10.

Kwenye Golden Glove hakuna vita inayoshindaniwa leo, kwani kipa wa Arsenal, David Raya alishanyakua baada ya kucheza mechi 15 bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa.

MECHI ZA MWISHO LIGI KUU ENGLAND MSIMU WA 2023-24

Arsenal vs Everton

Brentford vs Newcastle

Brighton vs Man United

Burnley vs Nottm Forest

Chelsea vs Bournemouth

Crystal Palace vs Aston Villa

Liverpool vs Wolves

Luton Town vs Fulham

Man City vs West Ham

Sheffield Utd vs Tottenham

Mechi zote zinachezwa Saa 12:00 Jioni.

Chanzo: Mwanaspoti