Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pazia la Championship kufungwa kibabe

Pazia Championship Pazia la Championship kufungwa kibabe

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pazia la Ligi ya Championship linatarajiwa kufungwa rasmi leo kwa viwanja sita kuwaka moto katika vita ya kupambana kusaka alama tatu za kuhakikisha kila mmoja inamaliza msimu kwa kuvuna kile ilichopanda.

Viwanja viwili havitachezwa kutokana na timu mbili kujitoa kwenye ligi, Ndanda ambayo leo ilipaswa kuwa nyumbani Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara dhidi ya Transit Camp sasa faida itabaki kwa maafande hao kupewa alama za mezani.

Pia mchezo kati Gwambina na JKT Tanzania nao hautacheza kutokana na sababu kama hizo na kuifanya JKT Tanzania kumaliza msimu kibabe zaidi ikiwa kileleni kwa alama 63.

Vita kubwa katika michezo ya leo itakuwa kwenye kupata timu moja ya kupanda daraja moja kwa moja kati ya Kitayosce inayoshika nafasi ya pili dhidi ya Pamba inayoshika nafasi ya tatu huku zikiwa zimepishana alama moja.

Shughuli nyingine ipo kwa kupata timu itakayomaliza nafasi ya nne kati ya Mashujaa yenye alama 46 nafasi ya nne dhidi ya KenGold inayoshika nafasi ya tano huku zikiwa zimepishana alama mbili.

Pale Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga napo kuna mchezo wa kukatana jasho wakati KenGold ikiwa inasaka alama tatu za kumpeleka nafasi ya nne wakati Biashara inasaka alama tatu ili kujinasua na janga la kucheza hatua ya mtoano kukwepa kushuka daraja.

Baada ya michezo ya leo timu itakayomaliza nafasi ya tatu na ile ya nafasi ya nne zitacheza hatua ya mtoano kusaka nafasi moja ya kupanda Ligi Kuu.

Timu itakayoshinda itangoja timu ya Ligi Kuu itakayofungwa kwenye hatua ya mtoano kati ya timu itakayomaliza nafasi ya 13 na 14 ambazo mchezo wa kwanza zitakutana Mei 31.

Timu ya Ligi Kuu itakayofungwa kwenye hatua ya mtoano itakutana na timu ya Ligi ya Championship itakayoshinda na mchezo wao wa kwanza utapigwa Juni 7.

Katika kumbukumbu za Championship timu ambayo iliwahi kufanikiwa kupanda Ligi Kuu kupitia mfumo huu ni Ihefu pekee ilipoichapa Mbao FC msimu wa mwaka 2020/21 ambapo timu tatu za Championship zilipanda daraja ikiwemo Dodoma Jiji na Geita Gold.

Kocha wa Kitayosce, Henry Mkanwa alisema wanaingia uwanjani kukipiga dhidi ya African Sports kwa tahadhari kubwa kwenye mchezo huo kwani alama tatu kwa timu zote ni muhimu.

Kocha wa Pamba, Yusuph Chippo alisema wataendelea kupambana hadi dakika za mwisho kuona namna timu yao itakavyomaliza msimu katika kutimiza lengo.

Huko Mashujaa FC, kocha Rashid Idd 'Chama' alisema umekua msimu bora kwao kumaliza nafasi ya juu msimu huu kutokana na kuwepo kwa kikosi bora lakini kikubwa ni kuhakikisha timu inamaliza nafasi ya nne.

Katika vita ya ufungaji bora, Edward Songo mshambuliaji wa JKT Tanzania mwenye mabao 18 ameweka wigo mkubwa kati yake na Fabrice Nyoy wa Kitayosce aliyecheka na nyavu mara 14.

Songo anayo nafasi kubwa ya kunyakua kiatu cha ufungaji bora kwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kuwa kinara kwa mabao yake 16, licha ya timui yake kushindwa kurudi Ligi Kuu baada ya kupasuka kwenye mchezo wa fainali ya Play-off na Tanzania Prisons.

Chanzo: Mwanaspoti