Pazia la michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 Bora linafunguliwa leo kwa mechi tano tofauti, huku vigogo Simba na Yanga zikiwa kwenye utata wa kucheza mechi ndani ya mwaka huu kutokana na kubanwa na ratiba ya viporo vya mechi za Ligi Kuu na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ugumu upo zaidi kwa Simba kulinganisha na Yanga, japo mabosi wa klabu hiyo wameweka wazi kuwa kwa sasa wanasubiri waendeshaji wa michuano hiyo TFF kupanga wacheze lini kutokana na muingiliano wa ratiba za timu hizo.
Simba ina mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa kesho Ijumaa kabla ya Jumanne ijayo kuumana na Wydad Casablanca ya Morocco, halafu itamalizana na KMC Desemba 23 kabla ya kusafiri hadi Kigoma kucheza na Mashujaa Desemba 26 na siku tatu baadaye itakuwa Tabora kuumana na Tabora United.
Januari Mosi, Simba itarudi Dar es Salaam kucheza mechi nyingine ya Ligi dhidi ya Azam kabla ya kusafiri hadi Zanzibar kwa michezo ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.
Kwa upande wa Yanga itashuka uwanjani Jumamosi kuvaana na Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu kabla ya Desemba 20 kucheza na Medeama katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Desemba 22 kuumana na Tabora United mjini Tabora na Desemba 29 itakwaruzana na Mashujaa.
Ratiba ASFC leo
Cosmopolitan vs Rhino Rangers (Uhuru)
Dodoma Jiji vs Magereza Dar (Jamhuri, Dodoma)
Ihefu vs Rospa FC (Highland Estate)
JKT Tanzania vs Kurugenzi (Azam Complex)
Coastal Union vs Greenland FC (Mkwakwani)