Majeraha bado yamekuwa tatizo kwa kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba katika kipindi hiki, baada ya ripoti kueleza wazi kuwa ni majeruhi tena.
Ripoti zinasema nyota huyo wa Juventus anaweza kukaa nje ya uwanja kwa hadi siku 30 kutokana na tatizo lake la sasa.
Tangu ajiunge tena na wababe hao wa Italia kutoka Manchester United Julai mwaka 2022, Pogba amekuwa akikabiliwa na majeraha akicheza michezo miwili pekee ambazo ni jumla ya dakika 35.
Sasa Juventus wamethibitisha kwamba Pogba mwenye umri wa miaka 29 amepata jeraha la kiwango cha chini kwenye paja lake la kulia na ameanza mchakato wa matibabu haraka.
Sky Italia imesema kuwa jeraha hilo la paja litamwacha Pogba nje ya uwanja kwa kati ya siku 20 hadi 30, hivyo atakosa michezo iliyosalia kabla ya mapumziko yajayo ya kimataifa, pamoja na nafasi ya kuiwakilisha Ufaransa katika michezo ya kufuzu Euro.
Bila Pogba, Juventus walishinda 4-2 katika mchezo wao wa Serie A dhidi ya Sampdoria Jumapili (Machi 12), huku Adrien Rabiot akifunga mara mbili kwenye mechi hiyo.