Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Patson Daka awe somo kwa Watanzania

Patson Daka.jpeg Patson Daka awe somo kwa Watanzania

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni dakika ya 88, mechi ya pili ya hatua ya makundi kwa Tanzania na Zambia. Tanzania inaongoza 1-0 kwa bao la mapema la Saimon Msuva na Zambia inapata kona.

Clatous Chama anaichonga vizuri na Patson Daka anakimbia kutoka kwenye nukta ya kupigia penalti kuelekea nguzo ya kwanza.

Anakutana na mpira na kupiga kichwa maridadi kinachomshinda kipa Aishi Manula na mpira kujaa wavuni… Zambia inasawazisha!

Kama siyo Patson Daka, Tanzania ingeandikisha ushindi wa kwanza kwenye AFCON, katika historia yake.

Zinaongezwa dakika saba, hakuna kilichobadilika. Mpira unaisha na Daka anatangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi.

Ni nani huyu Patson Daka? Patson Daka ni mchezaji aliyeibuliwa na programu ya Airtel Rising Stars mwaka 2012  Zambia, yeye na mwenzake Enock Mwepu ambaye sasa ameacha mpira kutokana na matatizo ya moyo.

Baada ya kupatikana, bwana mmoja wa kuitwa Lee Kawanu aliyekuwa akimiliki akademi ya Kafue Celtic, akawachukua na kuwalea kwenye akademi yake.

Wakawekwa kwenye kikosi cha Zambia kilichoshinda ubingwa wa U-20 wa Afrika 2017 na kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia.

Frederick Kanoute, nyota wa zamani wa Mali na klabu za Tottenham Hotspur na Sevilla, akawachukua na kuanza kuwasimamia.

Yeye ndiye aliyewauza kwenda RB Salzburg ya Austria na baadaye kuwapeleka England, Leicester City (Daka) na Brighton (Mwepu).

Uhamisho wao kwenda England ukaipatia Kafue Celtic zaidi ya Shilingi za Tanzania 20 bilioni kama fidia ya gharama ya kuwaendeleza wachezaji hao, kutokana na sheria za FIFA.

Kwa kifupi ni kwamba FIFA inaagiza timu yoyote iliyohusika kumuendeleza mchezaji kupata asilimia fulani ya mauzo kila anapouzwa kama fidia ya gharama walizotumia.

NI HIVI FIFA imetengeneza sheria kadhaa zinazohusika na uhamisho wa wachezaji. Sheria hizi zinalenga kuzinufaisha klabu zilizowekeza fedha, muda na maarifa katika kuwaendeleza wachezaji, pale wanapouzwa.

Kuna malipo  ya aina mbili 1. Fidia ya mafunzo Fidia ya mafunzo ni malipo yanahalalishwa na ibara ya 20 ya sheria za FIFA inayohusu hadhi na uhamisho wa wachezaji (RSTP).

Malipo haya yanaweza kudaiwa katika nyakati mbili, wakati wa maisha ya soka ya mchezaji husika.

i. Pale mchezaji anaposaini mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa. ii. Kila wakati mchezaji anapohama kutoka klabu moja kwenda nyingine kabla hajavuka miaka 23.

2. Malipo ya mshikamano Kwa mujibu wa ibara ya 21 ya sheria za FUFA kuhusu hadhi na uhamisho wa wachezaji, malipo ya mshikamano ni yale yanayotokea pale mchezaji ambaye bado ana mkataba na anauzwa kwenda klabu nyingine.

Asilimia hadi tano ya ada ya uhamisho hukatwa na FIFA moja kwa moja kwa ajili ya timu zilizohusika kumuendeleza mchezaji kuanzia akiwa na miaka 12 hadi 23. Haya ndiyo huitwa malipo ya mshikamano na hugawanywa kulingana na muda ambao mchezaji husika alikaa kwenye hizo timu zilizomuendeleza.

Na hii haina mwisho. Hilo fungu litaendelea kutoka kila wakati mchezaji atakapouzwa…hadi atakapostaafu.

Muda huu Kafue Celitc wanaombea Daka auzwe kutoka Leicester kwenda klabu nyingine ili wavune mijihela mingine.

SOMO Mpira ni biashara nzuri sana endapo itafanywa kimkakati. Katika nchi kama Tanzania ambayo watu huanzisha timu ili tu kushindana na Simba na Yanga, inatakiwa elimu kubwa sana ya ujasiliamali wa mpira kuwaelewesha kuwekeza ili kutengeneza pesa.

Badala ya watu kuanzisha timu yao mkoani huko ili wazione Simba na Yanga, waanzishe timu ili kuzalisha wachezaji wa kuwauza na kupata pesa.

Soko la wachezaji ni kubwa na linazidi kuongezeka. Mataifa mengi ya Asia ambayo yameimarika kiuchumi, yanataka kuimarisha ligi zao kibiashara.

Hii ina maana kwamba watahitaji wachezaji wazuri ili kufikia malengo. Endapo utafanyika uwekezaji wa viwango kuanzia ngazi za chini kabisa, Tanzania inaweza kuzalisha kina Patson Daka wengi mno; Hapa taifa litaweza kufaidika na wawekezaji pia wakafaidika kwa kuingiza pesa nyingi sana!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live