Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Patrick Benjamin mbongo aliyepita Simba, ammezea mate Gavi

Patrick GGG Patrick Benjamin mbongo aliyepita Simba, ammezea mate Gavi

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pablo Gavira maarufu kama Gavi ameingia moyoni mwa mashabiki wa Barcelona, humwambii kitu Xavier Hernandez 'Xavi' juu ya uwezo wake na hata wakati wa Kombe la Dunia kule Qatar tulishuhudia alivyokuwa mhimili mkubwa wa Hispania eneo la kiungo chini ya Luis Enrique.

Ndivyo anavyotamani iwe hivyo Patrick Benjamin aliyeko Hispania na kamchagua fundi huyo kama mfano kwake akiwa akiwa na akademi ya SPAIN RUSH-SPF.

Benjamin mwenye miaka 19, ni kiungo Mtanzania mwenye ndoto ya kucheza Ligi Kuu Hispania 'La Liga' na hapa anaeleza safari yake ya soka hadi kufika Ulaya na anavyotamani kukutana na Gavi ambaye licha ya kuwa na umri mdogo ni mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Barcelona.

"Gavi ni fundi sana, amekuwa akifanya vizuri na ametuonyesha vijana wenzake kuwa inawezekana licha ya kuwa na umri mdogo kucheza kwenye vikosi vya kwanza, ni shauku yangu kuanza kucheza soka la kulipwa nikiwa na umri mdogo."

"Najua ni ngumu kwa wachezaji wengi wa Kiafrika, yote hiyo ni kutokana na kukosa misingi bora ya soka angali tukiwa na umri mdogo kabisa tofauti na wenzetu huku Ulaya, lakini kuwa kwangu hapa kutanisaidia kukua na kupigania hilo, siku zote nimekuwa nikiamini penye nia pana njia," anasema.

Anaendelea kusema; "Navutiwa sana na Gavi kwa vitu vingi, aina ya soka lake amekuwa akitumia akili zaidi kuliko nguvu, ni mchezaji wa kitimu zaidi, bado sijapata nafasi ya kuonana naye nikiwa hapa (Hispania) lakini najua kuwa ipo siku na nitapata nafasi ya kuongea naye."

Gavi alizaliwa Los Palacios ya Villafranca, Andalusia. Alianza uchezaji wake akiwa na La Liara Balompie, ilikuwa ni klabu katika mji wake wa asili, alikaa miaka miwili, kati ya 2010 na 2012. Kutoka hapo alihamia akademia ya vijana ya Real Betis, ambako alikaa kwa misimu miwili. Alifunga mabao 95 kwa timu ya vijana ya Real Betis.

Mnamo mwaka 2015, akiwa na umri wa miaka 11, alijiunga na Barcelona kama mchezaji chipukizi ambaye alikuwa akicheza kikosi B. Septemba 2020, alitia saini mkataba wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa na klabu hiyo, na akapandishwa moja kwa moja kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 16 hadi timu ya chini ya miaka 19.

Alianza kuchezea Barcelona B Februari 21, 2021, katika mchezo wa nyumbani wa 6-0 wa L'Hospitalet, akitokea kama mbadala wa Nico Gonzalez katika dakika ya 77. Tangu hapo uwezo wake ukawa gumzo na kuanza kutumika hadi kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya soka la Hispania na hatimaye timu ya taifa.

Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Gavi, Benjamin anatueleza safari yake ilipoanzia akiwa Tanzania hadi kufika Hispania ambako mbali na soka anapiga kitabu kama ambavyo imekuwa kwa wachezaji wengi wakubwa barani humo.

"Nimezaliwa mkoani Mbeya (Uyole) na ni mtoto wa mwisho katika familia ya mzee Benjamin Mwandete kati ya watoto wanne. Safari ya soka ilianzia Shule ya St Patrick High School nikiwa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne mwaka 2020."

"Mwaka 2021 nilienda kufanya majaribio Simba timu ya vijana chini ya miaka 17 na nilibahatika kukaa hapo kwa mwaka mmoja, baada ya kufanya vizuri hapo wazazi wangu walivutiwa na uwezo wangu na kuona kuna haja ya kupigania ndoto zangu," anasema kinda huyo.

Anaendelea kueleza kwa kusema; "Baada ya hapo ndio Baba yangu mzazi alinitafutia nafasi huku Hispania kwenye akademi ambayo ipo Valencia, lakini mtu pekee aliyewezesha na kusaidia kupata nafasi hii ni Mr Seif Mpanda ambaye huku wapo watoto wake watatu, Barka, Jabir na Tariq Seif,"

"Pia kipengee nitumie nafasi kumshukuru Mr Seif Mpanda na Hemed Tawah kwa kufanikisha safari yangu nzima kufika hapa SPF Academy na bado wanaendelea kuniongoza katika njia bora na sahihi za kuweza kutimiza ndoto zangu na pia niushukuru uongozi wa SPF kwa kuendelea kunilea na kunipa mafunzo bora."

Mbali na soka, anaeleza amekuwa akiendelea na masomo ya kawaida ikiwa ni pamoja na kukijua vizuri Kihispania ili iwe rahisi kwake kufanya mawasiliano akiwa na wenzake nchini humo.

"Ninafuraha na maisha ya soka ya Hispania, hakuna changamoto kubwa ambayo nakutana nayo zaidi nimekuwa msikivu na mwenye kupenda kujifunza ili nifanikishe ndoto zangu," anasema Benjamin.

Katika moja ya ndoto za Benjamin mbali na kukutana na Gavi, kucheza La Liga anatamani pia jina lake kuimbwa Tanzania kutokana na kile ambacho anafanya kama ambavyo imekuwa kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

"Napenda kazi yangu ionekana, natamani kuona wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wakijivunia mimi, hilo limekuwa kichwani mwangu," anasema.

Chanzo: Mwanaspoti