Vuguvugu la ‘Ole Out’ lilifikia tamati wikiendi iliyopita. Uongozi wa Man United umeamua kumtimua na kuanza safari upya.
United kwa sasa ipo chini ya Michael Carrick ambaye alikuwa ni msaidizi wa Ole Gunnar Solskjaer. Swali ni kwamba, Nani atakwenda kuchukua nafasi ya kuiongoza Man United.
Baadhi ya makocha wanatajwa kwenye kinyang’anyiro cha ukocha pale Old Trafford. Kati ya wengi, haya ndio majina yanayopewa nafasi:
Mauricio Pochettino:
Kwa mashabiki wa EPL hili sio jina geni. Safari yake aliianza pale Southampton kabla ya kutua Spurs na sasa yupo PSG. Pochettino anasifika kwa uwezo wa kuongoza timu kwa kuhitaji kila mchezaji kuonesha uwezo wake thabiti.
Hakika, timu ya Pochettino lazima iwe na nguvu kubwa ya kushambulia. Amehusika katika kukuza wachezaji wakubwa kwenye soka kwa sasa, Sadio Mane, Van Djik, Harry Kane, Delle Ali, Luke Shaw ni miongoni mwa wachezaji waliopita kwenye mikono yake.
Zinedine Zidane:
Zidane hana timu kwa sasa tangu alipoondoka Real Madrid. Japokuwa inasemakana hana mpango na Man United. Lolote linaweza kutokea.
Zizzou hana mfumo maalumu wa kuichezesha timu uwanjani lakini, ni kocha anayeamini kwenye njia rahisi za kupata ushindi. Unaweza usielewe kikosi chake lakini anauwezo wa kukupiga magoli mengi ndani ya mechi moja.
Umwamba wa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara 3 mfululizo ndio kitu kinachomueka kwenye ramani mpaka sasa.
Erik Ten Hag:
Mtaalamu wa soka kutoka Uholanzi. Aliwahi kufanya kazi na Pep Guardiola pale Bayern Munich. Sasa hivi anafanya kazi na Ajax kama kocha mkuu.
Alifanikiwa kuifikisha timu hiyo kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, ametwaa mataji 2 ya Ligi Kuu nchini Uholanzi na msimu huu, ameshafuzu hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa akiwa na michezo 2 mkononi.
Falsafa yake ya kushambulia na kukuza vipaji vya wachezaji, ni faida kwa Man United.
United itamchagua nani kati ya hawa?