Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Papy Tshishimbi : Kuna mambo matatu nimejifunza kwa nyota wazawa

99589 Papii+pic Papy Tshishimbi : Kuna mambo matatu nimejifunza kwa nyota wazawa

Fri, 20 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

MMEZOEA kuniona uwanjani. Lakini nina kipaji vilevile cha uchambuzi ambapo kuanzia leo Alhamisi nitakuwa napatikana ndani ya Mwanaspoti nikifafanua mambo mbalimbali ya kimichezo na kutoa elimu ya hapa na pale kwa wanamichezo wenzangu.

Kwahiyo wadau wa michezo msikose kunifuatilia kwenye ukurasa huu kila siku ya Alhamisi.

Nimekuwa Tanzania kwa mwaka wa tatu sasa nikiichezea klabu ya Yanga na uwepo wangu hapa umenifanya nikutane na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wakija kuongeza nguvu wakishirikiana na wazawa wengi wenye uwezo na vipaji vya aina yake ambao tumewakuta hapa.

Hivi karibuni Watanzania wengi na wengine ambao sio Watanzania niliwaona jinsi walivyokuwa wanajazana katika runinga mbalimbali wakimfuatilia nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anavyocheza kule England katika klabu yake ya Aston Villa.

Watanzania wamekuwa wakifanya hivyo sio tu kwa vile Samatta yupo England, lakini wapo wengi walikuwa wakimfuatilia nyota huyo tangu alipokuwa Genk ya Ubelgiji, ila mwamko zaidi ukaja alipohamia Villa katika ligi ambayo inafuatiliwa na wengi.

Hi ni ishara kwamba wengi wanatamani kuona mafanikio zaidi kwa wachezaji wao wengine nje ya mipaka ya Tanzania. Wanatamani kuona wikiendi moja wakikaa kwenye runinga wanashuhudia wachezaji kadhaa wakicheza wengine Ufaransa, Ujerumani na kwingineko.

Pia Soma

Advertisement
Kiu yao hii kubwa ina maana moja kwamba kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi hili ingesaidia kuboresha zaidi timu yao ya taifa katika kupiga hatua zaidi na kuwa na wachezaji wengi bora zaidi.

Nasema hivi nikiangalia taifa kama la kwetu la DR Congo, ninalotokea mimi, tumekuwa tukiheshimika zaidi katika soka la Afrika na hata dunia kutokana na kuwa na wachezaji wengi wanaotoka nje wakicheza soka la kulipwa sehemu mbalimbali duniani.

Idadi hiyo imekuwa ikiifanya timu yetu ya taifa kuwapatia makocha wigo mpana wa kuchagua yupi mchezaji bora na hata kikosi kinapoitwa bado wako wachezaji wengi wanabaki wakikosa nafasi kitu ambacho kinaongeza ushindani. Wakati mwingine inakuwa vigumu kwa staa wa ndani ya Afrika kuonekana kwa maana ushindani ni mkubwa sana na wanaotoka Ulaya kwenye klabu kubwa ni wengi.

Wanazidiwa ubora au uzoefu na wale ambao wanacheza soka nje ya DR Congo lakini pia hilo limekuwa likituathiri kundi lingine ambalo hata mimi nipo licha ya kucheza nje lakini bado sijafanikiwa kupata nafasi kama hiyo.

Nilipofika hapa katika kuangalia kwangu nikaona mambo mengi ambayo wachezaji wa hapa Tanzania wanatakiwa kuyafanya ili kuongeza idadi ya wachezaji wa kulipwa nje ya nchi yao.

Jambo la kwanza ambalo nimeligundua wachezaji wengi wazawa wanaogopa kufanya kazi na makocha wa kigeni au wapo ambao pia hawawapendi kabisa.

Hili limekuwa likiwapa shida wachezaji wengi hapa licha ya kuwa na vipaji unaweza kukuta mchezaji mzuri anajua lakini akiona kocha mgeni ghafla hali yake ya kujiamiani inapotea anabadilika na kuanza kuonekana mchezaji wa kawaida. Siwezi kusema labda inatokana na utofauti wa lugha ambayo makocha hawa wanakuja nayo lakini nimeona wengi wanashindwa kufanya kazi vizuri na matokeo yake wanapoteza ushawishi mzuri kwa makocha hawa, hili ni lazima walifanyie kazi.

Hata wakienda nje lazima watakutana na makocha wa kigeni kama ambavyo hata mimi nimekutana nao. Kutokujua Kiingereza sana hakujanifanya nishindwe kuonyesha ubora wangu hii ni lugha tu ambayo unaweza kujifunza na kuielewa kama utaweka mkazo na juhudi binafsi ili uweze kurahisisha mawasiliano.

Jambo la pili ambalo nimegundua hapa wachezaji wengi wanapenda kusikiliza nini watu au mashabiki wanasema juu yao.

Nilipofika Tanzania nakumbuka watu wengi walinielewa wakati nilipocheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya Simba niliona kila shabiki alifurahia baada ya hapo kuna wakati nilishuka kidogo kwa sababu mbalimbali wapo ambao waliongea mambo mengi mabaya kuhusu mimi.

Sikutaka kuyaweka sana katika akili yangu hayo yote niliyapuuza nikaweka mkazo katika kuongeza juhudi katika mazoezi na sasa niko sawa.

Hili limekuwa gumu kwa wachezaji wa hapa Tanzania wengi wamekuwa wakipenda kusikiliza nini mashabiki wanasema.

Kama ukifanya kosa la kuruhusu yanayozungumzwa kuingia katika akili yako kama hauna ujasiri unaweza kupotea.

Jambo la tatu ambalo linaweza kuwa muhimu zaidi ni kwamba wachezaji wengi wa hapa hawapendi kuthubutu kufanya kitu tofauti katika maisha.

Ukiwa unacheza soka lazima uwe na uthubutu wa dhati na moyo wa kupambana.

Unaweza kutoka nyumbani katika nchi yako unakwenda sehemu nyingine ambayo hukuwa umewahi kwenda.

Sio kama ukifika huko utakuta kila kitu rahisi, unatakiwa kupambana uweke juhudi katika kila ugumu utakaokutana nao.

Tanzania ina wachezaji wengi wazuri ambao naamini wakiyafanya mambo haya matatu wanaweza kutoka nje na kwenda kucheza klabu mbalimbali Ulaya na kwingineko kisha kuzidi kulipa faida kubwa taifa lao.

Kwa leo nakomea hapa ila nawaomba sana mashabiki na wadau wote popote mlipo mchukue tahadhari kubwa dhidi ya virusi hatari vya Corona. Mimi najilinda, wewe jilinde na familia yako na wote wanaokuzunguka.

Chanzo: mwananchi.co.tz