Wakati wowote Coastal Union inaweza kuachana na kocha wake Mwinyi Zahera Mwanaspoti linafahamu kwa undani.
Taarifa kutoka ndani ya Coastal Union ni kwamba Zahera amezuiwa kujiunga na timu hiyo iliyopo Mbeya kwa ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara.
Coastal Union tayari imetua jijini Mbeya leo Oktoba 18 ikijiandaa kupambana na wenyeji wao Ihefu kwenye mchezo wa sita wa ligi huku Zahera akikwama jijini Dar es Salaam.
Mwanaspoti linafahamu kuwa Zahera awali ilipangwa asafiri na ndege lakini amepigiwa simu na bosi mmoja wa juu wa klabu hiyo akitakiwa kubaki jijini Dar es Salaam akisubiri maelekezo ya kikao na mabosi wa wa klabu hiyo.
Mashaka ya ajira ya Zahera yanachangiwa na vuguvugu la timu hiyo kutoshinda hata mechi moja tangu kuanza kwa msimu wakipoteza tatu na kutoa sare mbili ikiwa mkiani chini ya msimamo wa Ligi.
Kuna nafasi kubwa timu hiyo itacheza mchezo ujao dhidi ya Ihefu bila ya kocha huyo huku mabosi wake wakijipanga kumtupia virago Mkongomani huyo.