Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Panga pangua ratiba TPLB ilivyoziharibia timu

Yanga Vs Kagera Panga pangua ratiba TPLB ilivyoziharibia timu

Wed, 24 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) juzi ilitoa taarifa ya kuahirishwa kwa michezo ya mzunguko wa 29 ambayo ilikuwa ichezwe kesho katika viwanja saba huku mchezo baina ya Mbeya City dhidi ya Yanga ukipelekwa mbele hadi Juni 6.

Katika taarifa ya TPLB ilieleza michezo ya mwisho itachezwa Juni 9 badala ya Mei 28 huku michezo ya mzunguko wa 29 itapigwa Juni 6 ili kutoa nafasi kwa Yanga inayojiandaa na michezo ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.

"Bodi inatambua kuwa klabu zilianza kufanya maandalizi ya michezo hiyo kwa tarehe zilizotangazwa awali na kwa masikitiko inafahamu kuwa mabadiliko haya yanaweza kuathiri maandalizi hayo kwa namna moja au nyingine.

"Hata hivyo Bodi inapenda kuufahamisha umma kuwa imelazimika kufanya mabadiliko hayo kwa maslahi mapana ya ligi na mpira wetu kwa ujumla," ilieleza taarifa hiyo ya TPLB.

Katibu mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema wao tayari timu ilishatua Lindi tangu walipomaliza mchezo wao dhidi ya Yanga na mabadiliko hayo yamewashtua.

"Tumekaa huku siku nyingi na hata tukisema tutabaki bado tunaona haitasaidia kitu hivyo tutafanya kikao ili tuone tunafanya nini ili kuirudisha timu Dodoma."

Katibu wa Polisi Tanzania, Michael Mtebene alisema wao waliishia Korogwe wakielekea Dar es Salaam kucheza dhidi ya Simba baada ya kuona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii juu ya kubadilika kwa ratiba.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema kikosi chao tayari kilitua Manungu tangu juzi lakini sasa wanajiandaa kurudi tena Kagera kwaajili ya maandalizi mengine.

KMC iliyokuwa inajiandaa na Tanzania Prisons timu ilitua Makambako tangu Mei 18 kwa kambi ya siku chache lakini baada ya taarifa hizo juzi kikosi hicho kikarejea Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Geita Gold, Constantine Moland alisema wao timu ilishaondoka kutokana na umbali uliopo kutoka Geita hadi Mbeya na taarifa iliwakuta wakiwa Singida hivyo ikawapasa warudi.

Kocha wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata alisema wao hawakuondoka lakini walikuwa kwenye hatua za mwisho za maandalizi kuelekea Singida kwaajili ya mchezo huo dhidi ya Singida Big Stars.

Chanzo: Mwanaspoti