Disemba ndo hiyo imezidi kunoga kwenye Ligi Kuu England huku makocha kibao wakivutavuta muda kabla ya kupigwa kibuti kutokana na mechi zao kuahirishwa baada ya maambukizi ya Uviko-19.
Kuachana na makocha ndicho kitu mabosi wa Ligi Kuu England wanaona ni suluhisho wakati timu zao zinapokuwa na wakati mgumu ndani ya uwanja. Watford ilikuwa klabu ya kwanza msimu huu kumpiga chini kocha wake ilipoachana na Xisco Munoz mwanzoni mwa Oktoba.
Kisha akafuatia Steve Bruce aliyefunguliwa mlango wa kutoka huko Newcastle United baada ya timu hiyo kuchukuliwa na matajiri wapya na ajira ya ukocha kwenye kikosi hicho kwa sasa inashikwa na Eddie Howe.
Akafuata Nuno Espirito Santo aliyepigwa kibuti na Tottenham Hotspur na nafasi yake kuja kuzibwa na Antonio Conte.
Na baada ya hapo, klabu tatu zaidi zilibadili makocha Norwich City ilimfuta kazi Daniel Farke, Dean Smith aliondoshwa Aston Villa na Manchester United ilimfukuza Ole Gunnar Solskjaer.
Baada ya hapo ziliibuka sura mpya kama za Eddie Howe, Steven Gerrard na Smith ambao wote wameshacheza mechi na wameanza vizuri.
Makocha wa Ligi Kuu England wanatafahamu wazi kwamba Desemba ni mwezi mgumu kwenye usalama wa ajira zao.
Kwa mujibu wa wacheza kamali huko kwenye Ligi Kuu England, wanafichua kwamba Rafa Benitez ndiye kocha aliye kwenye hatari zaidi ya kufutwa kazi huko Everton kwa sasa.
Lakini, vichapo vizito mfululizo kutoka kwa Man City na Arsenal zimemweka kocha Marcelo Bielsa kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kutimiliwa huko Leeds United. Klabu hiyo imekuwa kwenye mjadala wa kumbadili Bielsa baada ya mbinu zake kuonekana si nzuri, wakiruhusu mabao 11 katika mechi mbili za Ligi Kuu England.
Lakini, kocha wa Everton, Benitez ndiye aliyekwenye hatari zaidi hasa baada ya kuchapwa 4-1 na mahasimu wao, Liverpool.
Tangu kichapo hicho, Rafa alifanikiwa kupata ushindi mmoja tu wa mabao 2-1 dhidi ya Arsenal, ikiwa ni ushindi wake wa kwanza kwenye mechi saba za ligi. Alichapwa na Crystal Palace 3-1 na alitoa sare kibahati ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea.
Ralph Hasenhuttl huko Southampton yupo kwenye presha kubwa, kama ilivyo kwa Claudio Ranieri ambaye yupo kwenye klabu ya Watford, ambao wao kazi yao ni kuajiri na kufukuza.
Leicester City wamepungua ubora wake kwa msimu huu na jambo hilo linaiweka nafasi ya kocha Brendan Rodgers kwenye wasiwasi mkubwa.