Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Panga la Simba bado wawili baada ya Phiri

Phirii Goal.jpeg Moses Phiri

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwanaspoti linajua kwamba Simba inaendelea na mpango mkakati wa ndaaani sana ambao lengo lake ni kurejesha hadhi ya timu hiyo. Wanapitisha fagio moja la mastaa wasumbufu ndani ya kikosi hicho.

Yaani unaposoma hapa wao wanasema wamebaki watu wawili tu. Staili kama hiyo ya Simba iliwahi kufanywa na Yanga miaka michache iliyopita.

Habari kutoka ndani ya Simba ni kwamba wamefanya uchunguzi na kuona kuna kikundi cha mastaa watatu ambapo kama wakikimaliza tu basi makocha na timu nzima itafanya kazi kwa sauti na kwa nguvu moja kama ilivyo kauli mbiu yao.

Mastaa hao ambao wanaipasua kichwa Simba ni Clatous Chama ambaye kwa sasa yupo nje ya kikosi baada ya kusimamishwa akidaiwa kukwaruzana na mmoja wa makocha wa timu hiyo.

Wengine ni mshambuliaji Moses Phiri ambaye tayari imeshamuondoa kumpeleka kwa mkopo Power Dynamos ya Zambia na yule wa tatu ni Luis Miquissone.

Mastaa hao watatu Simba inataka kuwaondoa wawili kati yao ili kuvunja umoja wao wa ndani ya kikosi ambao umekuwa ukitajwa kuwa mgumu kufanya mambo yaende kwa wepesi.

Simba ilibakiza hatua chache tu kumtema Chama kwenye dirisha dogo la usajili ikitajwa kuwa ndio mwendelezo wa hesabu hizo, lakini ikakosa mtu sahihi wa kuziba nafasi yake ndani ya kikosi hicho.

“Yule Tchakei (Marouf) tungempata tungeachana na Chama. Imekuwa shida kidogo kuwa na hawa watatu. Miquissone hana shida sana, lakini tunaona kama anapokuwa na Chama na Phiri asingeweza kufanya kazi vizuri,” kilieleza chanzo chetu ndani ya Simba.

Za ndaaani kabisa zinasema kwamba, Simba inaona baada ya kusimamishwa kwa Chama, Miquissone ameanza kurejea kwenye ubora wake akijituma kwa nguvu ndani ya kikosi hicho.

Hesabu kubwa kwa sasa ni kuachana na Chama ambapo mabosi wa klabu hiyo wapo kwenye msako mkali wa kumsaka mrithi wake.

YANGA ILIPITA HUMOHUMO

Yanga ilipita katika njia hiyohiyo mara mbili wakati inajenga kikosi chake bora ilicho nacho ambacho kilichukua mataji yote kwa misimu miwili mfululizo iliyopita.

Mapema Yanga iliwatema kwa mpigo waliokuwa mabeki wake, Juma Abdul na Kelvin Yondani pamoja na kiungo Haruna Niyonzima kwa kugoma kuwaongezea mikataba ili kuondoa kundi lao.

Baada ya kuwaondoa kwa akili wakongwe hao mabosi wa Yanga waliingiza damu mpya ambazo ilikuwa rahisi kwa makocha wa timu hiyo kudili nazo kwa nidhamu.

Msimu uliopita Yanga pia iliendeleza hesabu hizo ikimtema winga wake Bernard Morrison kwa kugoma kumuongezea mkataba baada ya kudaiwa kuwa raia huyo wa Ghana ndiye anaondoa utulivu kwa kiungo mshambuliaji, Stephanie Aziz KI.

Baada ya kumuondoa Morrison, Azizi KI alitulia na haraka msimu huu raia huyo wa Burkina Faso aliuanza kwa kishindo akiwa na moto wa kufunga mabao na ndiye kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho na hata Ligi Kuu Bara akifunga mabao 10.

Chanzo: Mwanaspoti