Panga pangua kwenye safu ya benchi la ufundi katika timu za Ligi Kuu, tayari limepita timu 10 huku sita pekee ndio hazijafanya mabadiliko ya benchi la ufundi.
Timu ambazo hazijafanya mabadiliko ya benchi la ufundi ni Yanga, Geita, KMC, Singida Big Stars, Mbeya City na Mtibwa Sugar.
Hata hivyo makocha wa timu hizo ambao wamekaa kwenye nafasi zao kwa muda mrefu ni Nasreddine Nabi (Yanga) ambaye amedumu kwenye kikosi hicho tangu Aprili, 2021.
Nabi alichukua nafasi ya Cedric Kaze aliyetimuliwa Marchi 7 muda mfupi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania pale Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Msimu wake wa kwanza aliiongoza michezo tisa, akishinda saba sare moja dhidi ya Namungo ilipotoa suluhu, kisha ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Azam.
Mtunisia huyo ameandika rekodi ya kuiongoza Yanga michezo 49 ya ligi bila kupoteza kabla kufungwa 2-1 Novemba 29, 2022 dhidi ya Ihefu sasa timu yake inaongoza ligi ikiwa na alama 56 akisaka kutetea ubingwa.
Nabi amezifundisha timu kadhaa ikiwemo, Pont Donnaz Hone Arnad (Itali) Al-Ahli Benghazi (Libya), Al-Hilal na Al -Merrikh (Sudan) na Ismaily (Misri).
Kocha mwingine wa Ligi Kuu aliyedumu na timu yake ni Fredy Felix ‘Minziro’ ambaye alianza na kikosi hicho tangu Agosti 29, 2020 akitokea Mbao FC iliyokuwa imeshuka daraja.
Minziro alianza na Geita ikiwa Ligi ya Championship lakini baada ya kuipandisha mabosi wakampa timu, Etienne Ndayiragije.
Oktoba 23, 2021 uongozi ulivunja mkataba na Ndayiragije kufuatia kushindwa kufikia malengo waliyokubaliana baada ya kuiongoza timu kwenye michezo minne na kuondoka kwake kulimpa nafasi nyingine, Minziro.
Minziro amezipandisha Ligi Kuu timu tatu KMC, Singida United na Geita Gold ambayo ikiwa nyumbani Uwanja wa Nyankumbu timu hiyo haijawahi kupoteza mchezo wowote wa ligi tangu ikiwa Ligi ya Championship.