Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pan African yaanza kibabe ugenini

Pan African Pan African yaanza kibabe ugenini

Sun, 10 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

TIMU ya Pan African ya jijini Dar es Salaam imefanya kweli ugenini baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Copco Veteran FC katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi ya NBC Championship msimu wa mwaka 2023/2024 umepigwa leo Septemba 9, 2023 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa kuanzia saa 10 jioni.

Wenyeji Copco FC ambao ni msimu wao wa pili kwenye mashindano hayo, imekuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Kelvin John dakika ya 36 kipindi cha kwanza bao hilo limeipa Copco uongozi wa bao 1-0 dakika 45 za kwanza.

Kipindi cha pili, Pan African imeanza kwa nguvu ikisaka bao la kusawazisha na hatimaye dakika ya 60 juhudi zao zikazaa matunda baada ya mshambuliaji, Kika Rashid kuiandikia bao la kwanza na la kusawazisha kwa shuti la mguu wa kulia.

Nyota huyo ambaye amejiunga na Pan African msimu huu, akaiandikia tena bao la pili timu yake mnamo dakika ya 79 kwa kichwa akiunganisha vyema mpira wa krosi ambao mabeki wa Copco wameshindwa kuukoa.

Dakika nne baadaye, Copco Veteran FC ikasawazisha bao hilo dakika ya 83 kupitia kwa winga wake waliyemsajili msimu huu kutokea Tabora United, Abdulkarim Segeja ambaye ameichambua ngome ya Pan African na kuuzamisha mpira nyavuni. Huku, Copco FC ikiwa na matumaini ya walau kuvuna pointi moja katika mchezo wa kwanza nyumbani msimu, Pan African ikapigilia msumari wa moto kwa kupata bao la tatu na la ushindi ambalo limefungwa na Kika Rashid dakika ya 85 kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Nyota huyo akicheza mchezo wake wa kwanza wa kimashidano na Pan African amefunga hattrick (mabao matatu) katika mchezo huo na kuwa mchezaji wa kwanza kwenye Championship msimu huu kufunga hattrick.

Baada ya kichapo hicho, Copco itajiuliza tena katika mchezo ujao wa pili nyumbani itakapoikaribisha Cosmopolitan ya jijini Dar es Salaam Septemba 16, mwaka huu, huku Pan African ikitupa karata nyingine ugenini Septemba 15, mwaka huu itakapovaana na Pamba katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Chanzo: Mwanaspoti