Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba yenye historia kwenye uwanja wa historia

Pamba Jiji FC Promoted Pamba yenye historia kwenye uwanja wa historia

Thu, 23 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabingwa wa Tanzania 1990, Pamba FC kutoka Mwanza, ambao sasa wanafahamika kama Pamba Jiji, watautumia Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwa mechi zao za nyumbani kwenye ligi kuu msimu ujao.

Timu hiyo ya kihistoria ambayo imerejea ligi kuu baada ya miaka 23, sasa inamilikiwa na Halmshauri ya Jiji la Mwanza ambayo pia inamiliki uwanja huo wa kihistoria.

Timu ya kihistoria

Kabla ya kushuka daraja mwaka 2001, Pamba FC ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na mamlaka ya Pamba tangu ilipoanzishwa mwaka 1968, ilikuwa ikitumia Uwanja wa CCM Kirumba.

Pamba ilipanda daraja kushiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara mwaka 1984.

Ikajipambanua na kuwa timu tishio iliyoogopewa sana nchini kutokana na kukusanya kikosi imara na chenye wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Hii ikaifanya timu hiyo kuwa maarufu na yenye wafuasi wengi sana.

Mamlaka ya Pamba iliwekeza vya kutosha kwenye timu kiasi kwamba katika kilele chake, Pamba ilikuwa timu pekee nchini iliyokuwa ikisafiri na ndege binafsi ya kukodi kwenye mechi zake.

Timu zingine kama Yanga na Simba zilikuwa zikisafiri kwa mabasi na wakati mwingine kwa kukata tiketi kama abiria wa kawaida.

Na kuna wakati wachezaji walipanda mabasi tofauti na kukutana kwenye kituo cha mechi huko mkoani.

Lakini Pamba walikuwa wanakodi ndege ya mgodi wa almasi wa Mwadui Shinyanga, na kusafiri nayo kwenye mechi zake.

WALIDHULUMIWA Mwaka 1988 Pamba walikaribia kutwaa ubingwa wa ligi ya Muungano, lakini waliupoteza dakika za mwisho.

Moja ya sababu za kuupoteza ubingwa huo ambao ndiyo ulikuwa mkubwa hapa nchini, ni “dhuluma” waliyokutana nayo Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Malindi, timu nyingine kigogo wakati huo, baada ya Simba na Yanga.

Wakiongoza 2-1 hadi dakika za 80, taa zikazimwa uwanjani na mechi kusimama. Itakumbukwa kuwa Uwanja wa Amaan ndiyo pekee uliokuwa na taa hapa nchini na mechi zake nyingi zilifanyika usiku.

Mechi ikapangwa kurudiwa wiki tatu baadaye na Pamba kupoteza 2-0.

Hapa ndipo Pamba walipopotea maboya. Lakini hitimisho la ubingwa likawa kwenye mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya hawa hawa Malindi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Pamba wakapoteza mchezo huo kwa bao moja la Amour Aziz, lakini kwa makosa makubwa ya mlinda mlango wao Peter Mhina. Na kuanzia hapo kipa huyo akaondolewa kwenye timu akituhumiwa kuihujumu timu. Kama mechi ingeisha sare, Pamba wangekuwa mabingwa wa Tanzania.

Hata hivyo, walijipanga na mwaka 1990 wakafanikiwa kubwa mabingwa na kushiriki klabu bingwa Afrika mwaka 1991. Wakatolewa na Sports Club Villa “Jogoo” ya Uganda kwenye hatua ya 16 bora.

Kuonesha kwamba walitolewa na timu bora, Villa wakiwa na fundi bora kabisa Afrika Mashariki, Majid Musisi, walienda hadi fainali mwaka huo.

Lakini mwaka 1990, Pamba ilishiriki Kombe la Washindi Barani Afrika, na kuweka historia inayodumu hadi leo. Ilishinda kwa matokeo ya jumla ya 17-1 dhidi ya Anse-Aux Pins ya Sheli Sheli. Walishinda 5-0 ugenini na 12 - 1 nyumbani. Ushindi huu unabaki kuwa rekodi ya Afrika kwa ushindi mkubwa zaidi wa jumla.

Hata hivyo, Kombe la Washindi lilifutwa na CAF mwaka 2003 kwa kuunganishwa na mashindano mengine yaliyoitwa Kombe la CAF, na ndipo likazaliwa Kombe la Shirikisho ambalo nalo sasa linafutwa.

Nyamagana uwanja wa kihistoria

Uwanja wa Nyamagana ulijengwa kama kumbukumbu ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia iliyoanza 1938 hadi 1945. Jina lake la kwanza lilikuwa uwanja wa Ukombozi. Mei 1945 uwanja huo ulikamilika na kukabidhiwa kwa halmashauri ya mji wa Mwanza katika nyakati hizo za mkoloni Muingereza. Hata hivyo, kilichojengwa kilikuwa sehemu ya kuchezea tu, yaani pichi.

Mwaka 1950 halmashauri ya mji wa Mwanza ikajenga uzio wa seng’enge kuuzungushia uwanja huo katika maandalizi ya kupokea maandamano ya machifu waliokuwa wakipinga serikali ya mseto.

Mwaka 1960 likajengwa jukwaa la kwanza la chini (ground stand), kwa ufadhili wa Dkt. Williamson, aliyekuwa mmiliki wa mgodi wa madini ya almasi Mwadui.

Mwaka 1972, uwanja huo ukajengwa upya kwa ufadhili mwingine wa Dkt. Williamson na michango ya wananchi wa mkoa wa Mwanza chini ya uongozi imara wa mkuu wa mkoa Omar Muhaji. Ndipo ukajengwa ukuta wa matofali, kuwekwa viti kwa mara ya kwanza pamoja na chumba cha matangazo ya redio pamoja na vyoo.

Hii ilikuwa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Taifa mwaka huo, yaliyofanyika hapo!

Ukarabati mwingine mkubwa ulifanyika baadaye mwaka huo kwa kuwekwa nguzo za taa za kisasa za umeme (Mercury Vapour Lamps) kama maandalizi ya tamasha kubwa la mwanamuziki kutoka Zaire (sasa DRC), Luambo Lwanzo Makiadi maarufu kama Franco.

Mwaka 1974, mashindano ya kutafuta klabu bingwa ya taifa ambayo sasa ndiyo ligi kuu, yalifanyika Uwanja wa Nyamagana. Fainali ikazikutanisha Yanga na Simba katika mechi iliyoitwa Nyamagana Thriller. Hii ndiyo mechi ya kwanza ya watani wa jadi kufanyika nje ya Dar es Salaam.

Wakati wote huo uwanja huu ulikuwa chini ya mkurugenzi wa utamaduni wa taifa.

Mwaka 1979, umiliki wa uwanja huu ukahamishiwa kwa halmashauri ya mji wa Mwanza ambapo upo hadi sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live