Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba yazidi kuzoa pointi Nyamagana, Kocha atamba

Pamba Jiji Mwanza Pamba yazidi kuzoa pointi Nyamagana, Kocha atamba

Sat, 21 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Pamba Jiji imeendelea kuwa ngumu kufungika katika uwanja wake wa nyumbani, Nyamagana baada ya leo kuzoa pointi nyingine tatu ikiwachapa maafande wa Transit Camp ya jijini Dar es Salaam.

Pamba imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Transit Camp leo Oktoba 21, 2023 kwenye mchezo wa Ligi ya Championship ambao umepigwa saa 8 mchana katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa.

Licha ya ushindi huo, Pamba imeanza mchezo kinyonge ikitanguliwa kufungwa bao la mapema na wageni wao, kabla ya kurejea mchezoni na kupindua matokeo hayo.

Transit Camp wametangulia kupata bao dakika ya 29 likifungwa na Iddi Mbaga, lakini Pamba ikasawazisha bao hilo dakika mbili baadaye, dakika ya 31 kupitia kwa Ismaily Ally kwa shuti kali nje ya eneo la 18 na kumuacha kipa asijue la kufanya. Mabao hayo yamedumu kwa dakika 45 za kwanza na kwenda mapunziko wakitoshana nguvu.

Kipindi cha pili, Pamba imeanza kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne katika dakika ya 54 ikiwatoa Salum Kipemba, Rashid Mchelenga, Daniel Joram na Lazaro Mlingwa huku nafasi zao zikichukuliwa na Haruna Chanongo, Peter Mwalyanzi, Yusuph Adam na Michael Samamba, mabadiliko hayo yameongeza nguvu na kasi kwenye ushambuliaji na kuipa timu hiyo penalti dakika ya 60, lakini Haruna Chanongo akakosa baada ya kipa wa Tranist Camp kudaka shuti lake.

Dakika ya 58, Transit Camp imelazimika kucheza pungufu baada ya Kiungo wake, Khalid Misanga kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika matukio mawili ya kuzozana na mchezaji wa Pamba na kupiga mpira kwa hasira baada ya maamuzi ya refarii.

Mafaande hao wamefanya mabadiliko ya wachezaji wawili dakika ya 68 na 88 ikiwatoa Hussein Sindano na Sunday Justin na kuwaingiza Said Idozye na Baraka Jerome, huku Pamba ikiwatoa Aniceth Revocatus na kuingia Issah Ngoah dakika ya 73.

Mabadiliko hayo yamekuwa na matokeo chanya kwa kikosi Cha Pamba ambacho kimepata bao la pili na la ushindi dakika ya 79, likifungwa na Haruna Chanongo.

Ushindi huo ni wa nne msimu huu kwa Pamba katika ligi hiyo, na ukiwa wa nne katika uwanja wa nyumbani kati ya mechi tano ilizocheza, huku mchezo mmoja pekee dhidi ya ndugu zao wa Mwanza, Copco FC ukimalizika kwa suluhu (0-0).

Penalti iliyopata leo Pamba Jiji ni ya nne msimu huu katika mechi tano ilizocheza nyumbani, ambapo imepata penalti hizo katika mchezo dhidi ya Pan Africans, Cosmopolitan, Green Warriors na Transit Camp.

Bao ambalo imefungwa Pamba leo ni bao pekee ililoruhusu katika mechi tano za nyumbani, huku kipa wa timu hiyo, Raheem Sheikh akiwa na cleansheet nne katika mechi saba alizoidakia timu yake

Baada ya ushindi huo, Pamba inafikisha pointi 14 na kupaa kileleni sawa na TMA FC yenye pointi 14, humu Transit Camp ikibaki katika nafasi ya 14 na alama zao nne.

Kocha Msaidizi wa Pamba, Renatus Shija, amewataka mashabiki wa timu hiyo kuiamini na kuiunga mkono ili kutikiza lengo la kwenda ligi kuu huku akisisitiza kwamba timu itaendelea kupambana kushinda mechi zake kuliko kucheza kufurahisha watu.

Chanzo: Mwanaspoti