Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba yafunga mwaka kibabe

Pamba Jiji Fc Sq Pamba yafunga mwaka kibabe

Sun, 31 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Timu ya Pamba Jiji imeufunga mwaka 2023 kibabe kwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mbuni FC ya Arusha katika mchezo wa Ligi ya Championship.

Pamba imepata ushindi huo jana Desemba 30, 2023 katika mchezo wa raundi ya 15 ya ligi hiyo ambao umechezwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza kuanzia saa 10 jioni.

Mchezo huo ni wa kuhitimisha mechi 15 za mzunguko wa kwanza ni mwisho kwa Pamba Jiji kwa mwaka 2023 ambapo baada ya hapo inajiandaa na michezo mingine 15 ya mzunguko wa pili kuhakikisha malengo yake ya kupanda kwenda Ligi Kuu yanatimia.

Pamba imepata mabao yote matatu kipindi cha kwanza yakifungwa haraka haraka yakitokana na mipira ya kutenga, mabao mawili yamefungwa na Haruna Chanongo dakika ya  25 na 29, huku bao la tatu likifungwa na Michael Samamba dakika ya 39.

Baada ya mabao hayo, Kocha wa Mbuni, Leonard Budeba amefanya mabadiliko ya  wachezaji wawili dakika ya 40, akiwatoa Salum Rajabu na Shaban Hussein na kuwaingiza Ambokise Mwaipopo na Cassim Ally, ambao wamebadili mchezo na kuinusuru timu dhidi ya mvua ya mabao.

Pamba nayo imefanya mabadiliko dakika ya 50 ikiwapumzisha mfungaji wa mabao mawili, Haruna Chanongo pamoja na Peter Mwalyanzi na kuwaingiza Yusuph Adam na Jamal Mtegeta kisha ikamtoa Mudathir Said na kuingia Aniceth Revocatus, hata hivyo dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa Pamba kuondoka na ushindi wa mabao 3-0.

Ni ushindi wa pili mkubwa kwa Pamba katika Uwanja wa Nyamagana baada ya ushindi wa kwanza wa msimu wa mabao 4-0 dhidi ya Cosmopolitan, huku Mbuni ikikubali Kwa mara ya kwanza msinu huu kufungwa mabao matatu katika mchezo mmoja.

Baada ya ushindi huo, Pamba imefikisha pointi 31 katika nafasi ya tatu nyuma ya vinara, Ken Gold wenye alama 35 na Mbeya Kwanza inayokamata nafasi ya tatu na alama 32.

Kocha wa Mbuni, Leonard Budeba amesema kipindi cha kwanza vijana wake hawakucheza vizuri kwani wameshindwa kujipanga vyema na kukubali kufungwa mabao matatu ya haraka yaliyotokana na mipira ya faulo, lakini wakati wa mapumziko akazungumza na vijana wake kutaka wajirekebishe na wakafanikiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live