Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba yaendelea kuoga noti za RC Makalla

Pamba Msh(15).jpeg Pamba yaendelea kuoga noti za RC Makalla

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachezaji na benchi la ufundi la Pamba Jiji wameendelea kupokea mamilioni ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla kutokana na matokeo mazuri wanayoyapata kwenye Ligi ya Championship, huku akiwaahidi nyingine kama watazidi kumfurahisha.

Makalla ambaye ni mlezi wa timu hiyo, leo Januari 26, 2024 amewapa wachezaji na benchi la ufundi Sh5 milioni kama hamasa kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Biashara United na kuwataka kuhakikisha wanavuna pointi tatu.

Amekabidhi fedha hizo katika ukumbi wa ofisi yake jijini hapa wakati wa hafla ya chai na timu hiyo saa 4 asubuhi.

 Huo ni mwendelezo wa Mkuu huyo wa mkoa kutoa motisha kwa wachezaji wa timu hiyo wanapofanya vizuri ama wanapojiandaa na mechi, ambapo wiki iliyopita aliwapa Sh2 milioni ya motisha katika mchezo wao dhidi ya Stand United ambao walishinda kwa mabao 4-1.

“Nimeomba nikutane nanyi katika utaratibu wa kawaida ambao tumekuwa tukizungumza mazoezini, kwenye mechi na kambini nimeona tukutane kuelekea mechi na Biashara United, walitushindwa kwao hapa lazima waache pointi tatu,"

"Kuonyesha uwajibikaji wangu nawakabidhi Sh5 milioni ni hamasa kwa mechi iliyoko mbele yetu msiniangushe,” amesema Makalla

Hata hivyo, wakati akitoa motisha hiyo, Makalla ameuagiza uongozi wa klabu hiyo kuomba mchezo wao na Biashara United unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa (Jumapili) katika Uwanja wa Nyamagana, usogezwe mbele hadi Jumatano ijayo.

Hiyo ni kutokana na uwanja huo kuwa na matumizi mengine kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani humo ambapo atatumia uwanja huo kuzungumza na wananchi.

Mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Evarist Hagila, amesema niwahakikishie wananchi, viongozi na wachezaji kwamba hatutafanya makosa ya nyuma tutapanda daraja na amini ukame wa miaka 25 ambayo tulijaribu kupigana unakwenda kufika mwisho, tutahakikisha Pamba inakwenda kushindana na Simba, Yanga na Azam kama timu kubwa ya tatu nchini,”

Kocha wa Pamba, Mbwana Makatta, amesema hamasa zinazotolewa na viongozi hao zimekuwa chachu ya mafanikio kwa kikosi chake na kupelekea kazi yake kuwa rahisi, huku akimhahidi mkuu huyo wa mkoa kwamba wachezaji wana morali ya kupambana na watamfurahisha.

Mtendaji Mkuu wa Pamba, Alhaji Majogoro, amesema hamasa hizo ni deni kubwa kwa wachezaji na benchi la ufundi ambao inabidi walilipe na uongozi umejiandaa kuhakikisha lengo lake linafanikiwa.

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Aaron Kagulumjuli amesema kwa mipango waliyonayo ni lazima timu hiyo ipande daraja kwani hawafanyi majaribio uwanjani na kwa kikosi chao hakuna timu itakayowazuia kwani wamedhamiria msimu huu kuifanya historia ya timu hiyo iwe ya tofauti na miaka mingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live