Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba yaachana na kocha wake, kocha Biashara akaimu

Pamba Pic Kocha Pamba abwaga manyanga kwa matokeo mabovu

Tue, 28 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Klabu ya Pamba ya jijini Mwanza imeachana na kocha wake mkuu, Athuman Cairo kufuatia mwenendo mbovu wa matokeo ya timu hiyo katika Ligi ya Championship.

Pamba imeachana na Cairo baada ya kudumu klabuni hapo kwa mwezi mmoja na siku 17 tangu alipojiunga nayo Novemba 1, mwaka huu akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Cairo ameiongoza Pamba katika mechi saba za ligi akishinda mchezo mmoja, sare mbili na kupoteza mechi nne huku timu hiyo ikikamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 16.

Akitangaza uamuzi huo leo jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili, Aleem Alibhai amesema mwenendo usiyoridhisha wa timu hiyo tangu ikabidhiwe mikononi mwa kocha huyo ndiyo sababu kubwa iliyowasukuma kufanya uamui huo ambao umebarikiwa na kamati ya utendaji.

Amesema wamefikia pia uamuzi wa kuachana na kocha wa makipa Emmanuel Kingu baada ya kuona kuna udhaifu katika eneo hilo pia huku wakiendelea kulifanyia kazi na kulitazama benchi la ufundi.

Amesema wamemteua kocha wa makipa wa Biashara United ya Mara, Wilbert Mweta kuwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo wakati wakifikiria jina la kocha mpya.

“Jana kikao cha kwanza cha kamati yetu kiliketi na tumefikia maamuzi ya kusitisha mkataba wa kocha mkuu kutokana na mwenendo wa timu ambao siyo mzuri tangu ateuliwe kuwa kocha mkuu, tayari tumeshaanza kupokea wasifu wa makocha mbalimbali zaidi ya saba kutoka Uganda, Kenya na Tanzania tunakaribisha maombi zaidi na tutaendelea kuchuja majina kufika matatu ambayo tutayapeleka kamati tendaji kufanya maamuzi ya mwisho,” amesema Alibahi.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz