Pamba imeendelea kukusanya pointi tatu kwenye michezo yake ya Championship na kuzidi kujiweka katika nafasi za juu na kuweka hai matumaini ya kupanda daraja kwenda Ligi Kuu baada ya kukwama misimu iliyopita.
Baada ya kuichapa Copco FC mchezo wikendi iliyopita, leo Pamba imevuna pointi nyingine tatu nyumbani baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Biashara United ya Mara mchezo ukipigwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza kuanzia saa 10 jioni.
Pamba ambayo haikucheza vizuri ama kutengeneza nafasi nyingi za mabao katika mchezo huo, imepata ushindi huo kupitia bao pekee la Bruno John dakika ya 15 kwa mpira wa krosi uliozama kambani moja kwa moja na kudumu hadi dakika 90 za mchezo huo.
TP Lindanda baada ya kuifunga Biashara United leo inakuwa imelipa kisasi cha kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Oktoba 8, 2022 katika Uwanja wa Karume mkoani Mara.
Ushindi huo unaiimarisha Pamba katika nafasi ya tatu ikifikisha pointi 35 baada ya michezo 18, ikishinda 10, sare mbili na kupoteza tano, huku ikifunga mabao 22 na kuruhusu 15, wakati Biashara United ikibaki katika nafasi ya tisa na pointi zao 19.
Maafande wa JKT Tanzania ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 46 kufuatia ushindi wao wa leo wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya Kwanza ukiwa ni ushindi wao wa 15 msimu huu, sare moja na kupoteza mbili wakifunga mabao 28 na kuruhusu nane, huku Kitayosce ikikamata nafasi ya pili na pointi 41.
Ushindi wa leo ni wa pili mfululizo kwa Pamba baada ya wikendi iliyopita kuichapa Copco FC mabao 3-0 huku timu hiyo ikicheza michezo minne mfululizo bila kupoteza ikipata sare moja na ushindi mechi tatu.
Kocha wa Pamba, Yusuph Chippo amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo huku akitamba kuwa akili sasa inahamia kwenye mchezo ujao dhidi ya Pan African, wakati Kocha msaidizi wa Biashara United, Athuman Kairo amewapongeza Pamba na kuahidi kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana leo.