Timu za Pamba na Kitayosce ambazo zinawania nafasi ya kufuzu Ligi Kuu Bara msimu ujao juzi Jumamosi zilijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kubanwa mbavu na wapinzani wao ambao waliwakazia kuondoka na pointi tatu.
Timu hizo zilijikuta zikiambulia pointi moja kwenye michezo yao hiyo ambapo kwa upande wa Kitayosce wao walitoka suluhu na wenyeji wao Fountain Gate kwa kushindwa kufungana wakati Pamba wakiwa mkoani Tanga kucheza na African Sports walitoka sare ya bao 1-1.
Baada ya michezo hiyo, Kitayosce yenyewe imebakia kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 wakati Pamba wakiwa nafasi ya tatu na pointi 53, zote zikicheza mechi 29, huku JKT Tanzania wakiwa kileleni na pointi zao 63.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo ambayo ilipigwa juzi, JKT walibanwa mbavu na Mashujaa kwa kutoka sare ya kufungana mabao 3-3 na Mbeya Kwanza wakiwachapa Pan Africans kwa mabao 2-1.