Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba Jiji yaonywa mapema Ligi Kuu Bara

CxhgcxfdZfcgf Pamba Jiji yaonywa mapema Ligi Kuu Bara

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Maandalizi ya Pamba Jiji kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao wa mwaka 2024/2025 yanazidi kushika kasi, huku mastaa wa zamani na makocha wakiionya kufanya usajili wa kukurupuka utakaoisababisha kushuka daraja msimu wake wa kwanza.

Timu hiyo ya jijini hapa tayari imeachana na benchi la ufundi chini ya Mbwana Makatta na Renatus Shija walioipandisha daraja na kumleta kocha wa kigeni, Goran Kopunovic aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja.

Beki wa zamani wa Yanga na Toto Africans, Ladislaus Mbogo alisema klabu hiyo inapaswa kuwa makini katika usajili kwa kuleta wachezaji watakaoisaidia kubaki Ligi Kuu ili ijipange msimu ujao, huku akionya isijiwekee malengo makubwa ya ubingwa na nafasi tatu za juu.

“Mara nyingi timu zinazopanda zinashuka kwa sababu watu wanaojua mpira waliozipambania huwekwa pembeni na kuingia watu wasio na uchungu nazo, tumeona hili limeanza kuonekana Pamba, siyo mbaya kubadilisha uongozi lakini lazima uwe na matinki siyo mihemko,” alisema Mbogo na kuongeza;

“Watafute wachezaji wa kuifanya iendelee kuwa Ligi Kuu ili msimu unaofuata ndiyo walenge kushindana na kutafuta ubingwa. Ligi Kuu ina ushindani mkubwa na watu wanaojua njia za soka, Pamba ni lazima iwe makini.”

Mwenyekiti wa Chama cha Makocha (TAFCA) Mkoa wa Mwanza, Kessy Mziray alisema anaamini klabu hiyo ina watu makini watakaofanya usajili sahihi wakiwa wamepata somo kwa timu zilizoshuka na chama hicho kiko tayari kutoa ushauri wa kiufundi ukihitajika.

“Wasajili watu wanaotamani mafanikio na siyo ambao hawana tena njaa ya mafaniko, kwa hiyo watafute wachezaji wazoefu na wa kimataifa ili kupata ushindani na kufanya vizuri. Sisi hatutowaingilia ila wakihitaji ushauri milango iko wazi,” alisema Mziray.

Chanzo: Mwanaspoti