Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pamba, Copco hapatoshi Mwanza

Pamba X Copco Pamba, Copco hapatoshi Mwanza

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mashabiki wengine wakilipigia hesabu pambano la Ligi Kuu Bara linalopigwa kesho Jumamosi kati ya Geita Gold dhidi ya Yanga utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, upande wa Ligi ya Championship kuna vita nzito wakati Copco na Pamba watakapokutana Jumapili kwenye Mwanza Derby.

Pamba ndio wenyeji wa mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa ambapo awali mchezo huo ulipangwa kupigwa kesho Jumamosi, lakini ukasogezwa mbele kupisha pambano la Ligi Kuu ambalo Geita ndio wenyeji.

Katika mechi mbili za msimu uliopita Pamba ilikuwa mbabe baada ya kushinda zote, ambapo timu hizo zinakutana kesho huku Pamba ikiwa imevuna pointi saba katika michezo yake minne ikishinda miwili, sare moja na kupoteza mmoja huku Copco FC ikiwa na alama zake tatu baada ya kushinda mechi moja na kufungwa tatu.

Kiungo wa Copco FC, Ibrahim Njohole amesema mchezo huo utakuwa mgumu kwani wachezaji wanafahamiana na wanatoka jiji moja lakini kikosi chao kimejiandaa vizuri na kinaendelea na mazoezi huku benchi la ufundi likiendelea kuwaweka sawa kiakili na kimwili kwa ajili ya kufanya vizuri.

"Ni mechi muhimu kwetu kwasababu hatupo sehemu nzuri sana hivyo tunapaswa kupambana ili tuweze kutoka na matokeo mazuri, Pamba ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri ambao wengi wao wana uzoefu na wameshacheza Ligi Kuu lakini hiyo haiwezi kutuzuia kufanya vizuri hata sisi tuna wachezaji wazuri wenye uzoefu kama wao hivyo mechi itakuwa nzuri na ya kuvutia," amesema Njohole, huku nyota wa Pamba, Salum Kipemba alisema mtanange huo ni muhimu kwao kwani wanahitaji pointi tatu kwa udi na uvumba ili kunogesha safari yao ya kwenda Ligi Kuu huku akitamba kuwa baada ya kutofanya vizuri katika mechi mbili za ugenini dhidi ya Stand United na Biashara United wanazitaka pointi tatu za ndugu zao, Copco.

Kinara wa mabao wa Copco FC, Abdulkarim Segeja mwenye mabao matatu, amesema umuhimu wa mchezo huo kwao ni kupata pointi tatu na kuweka heshima kwani kushinda dabi kuna heshima yake na watapata ushindi kwani wanachukuliwa poa na ushindi utawarejesha hadi, licha ya kukiri Pamba wana ubora mzuri.

"Kwangu huanza kutanguliza timu kwanza ipate matokeo ila kwenye upatikanaji wa hayo matokeo ikitokea nimefunga nitashukuru Mungu na nitafurahi zaidi," amesema Segeja.

Chanzo: Mwanaspoti