Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pagumu! Faini Championship Sh20 milioni

JKT TZ SQUAD Vinara wa Ligi ya Championship, Kikosi cha JKT Tanzania

Wed, 15 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi ya Championship inaelekea ukingoni huku JKT Tanzania ikiendelea kusafisha njia ya kuhakikisha msimu ujao inacheza Ligi Kuu Bara baada ya kusota misimu miwili.

Hata hivyo, ligi hiyo iliingia dosari baada ya uongozi wa Gwambina kutangaza kujiondoa kutokana na kile walichodai kuonewa na mamlaka husika.

Januari 17, 2023 katika taarifa iliyotolewa na TFF iliwaelekeza wanasheria wake kuchukua hatua dhidi ya mmiliki wa Gwambina, Alexander Mnyeti kwa kutoa shutuma za uongo dhidi yake.

Katika taarifa hiyo ilieleza, Mnyeti kupitia moja ya kituo cha redio hapa nchini alisema aliwahi kuombwa Sh5 milioni ili wapate kibali cha kuutumia uwanja wao uliokuwa umefungiwa

Gwambina yachafua hewa

Katibu wa Gwambina, Daniel Kirai alitangza kujitoa kwenye ligi na wachezaji kuruhusiwa kuondoka kambini kwa kupewa barua za kuwa huru na benchi la ufundi kuvunjwa kwa madai ya kuonewa.

Mambo yalianza kwenda sivyo baada ya taarifa ya TPLB ya Novemba 2, 2022 kwa kuufungia Uwanja wa Gwambina na Ali Hassan Mwinyi na kuifanya Gwambina FC kwenda kuutumia Uwanja wa Nyamagana, Mwanza lakini mabosi wao hawakukubaliana na hilo.

Gwambina ikatozwa faini Sh 500,000 kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani katika mchezo dhidi ya Ndanda, ikatozwa tena faini kama hiyo kwa kosa hilohilo kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa michezo yote ilichezwa Nyamagana.

Oktoba 25, Gwambina ikatozwa tena faini Sh500,000 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia mawe waamuzi kwenye mchezo dhidi ya Pamba uliochezwa uwanja huo.

Pia meneja wa Uwanja wa Gwambina, Hobert Kabelinda na katibu wake, Jumanne Shija wakafungiwa miezi mitatu na faini Sh500,000 kila mmoja kwa kosa la kuingia chumba cha waamuzi na kuwatishia.

Baada ya mchezo dhidi ya Copco, afisa usalama wa Gwambina, Mrisho Yusuph alifungiwa miezi mitatu na faini Sh500,000 kwa kosa la kutoa lugha ya vitisho kwa waamuzi.

Gwambina ikapigwa faini Sh2 milioni na kupokwa alama 15 baada ya kushindwa kwenda uwanjani katika mchezo dhidi ya Mbuni, Gwambina ikapigwa faini Sh2 milioni na kupokwa alama 15 baada ya kushindwa kwenda uwanjani katika mchezo dhidi ya African Sports.

Pia Gwambina ikapigwa faini Sh2 milioni na kupokwa alama 15 baada ya kushindwa kwenda uwanjani katika mchezo dhidi ya Fountain Gate, na kufanya jumla ya faini Sh9 milioni, viongozi wakitozwa faini Sh1.5 milioni na timu Sh7.5milioni.

FAINI KAMA ZOTE

Hadi Machi 9, 2023 Ligi ya Championship imepigwa faini zaidi ya Sh20 milioni kutokana na makosa mbalimbali ambayo yamefanywa na wachezaji, mashabiki na hata viongozi wa timu.

Ukiachana na Gwambina ambayo hadi inajitoa kwenye ligi ilishapigwa faini ya Sh 9 milioni, Biashara United nayo ilikuwa ishapiga faini Sh1.5 milioni sawa na JKT Tanzania huku Mbuni FC ikipigwa Sh3.5 milioni.

Green Warriors yenyewe ishawatoka Sh3 milioni, Mbeya Kwanza Sh1 milioni wakati Fountain Gate wao wamepigwa Sh 500,000 kwa kosa la mashabiki wao kutoa lugha chafu kwa waamuzi wa mchezo dhidi ya Ndanda FC. Hizi ni baadhi tu ya faini zilizotolewa.

WAAMUZI NI BALAA! Katika faini ambazo timu zimekuwa zikitozwa zimekuwa zikihusisha waamuzi kwa kushutumiwa kupindisha sheria za soka kwani katika mchezo Namba 65 Biashara United dhidi ya Kitayosce mashabiki wa Biashara walimtolea lugha chafu mwamuzi wa mchezo huo na kurusha mawe kwenye paa kabla ya kuanza mchezo na mwisho wa siku timu kutozwa faini ya Sh 500,000.

Waamuzi waliochezesha mchezo namba 76 kati ya Mbuni na JKT Tanzania walishambuliwa baada ya mchezo kumalizika na mashabiki pamoja na katibu wa timu ya Mbuni, Michael Yoel naye akihusishwa na timu kutozwa faini ya jumla Sh 2.5 milioni.

Mwamuzi namba mbili katika mchezo wa Biashara dhidi ya KenGold alitolewa lugha ya matusi na mmoja wa walinzi (steward) wakati mchezo ukiendelea na mashabiki kutoa vitisho kwa waamuzi jambo lililosababisha washindwe kutoka uwanjani kwa wakati na timu hiyo kutozwa faini ya jumla Sh 2.5 milioni.

Biashara ni moja ya timu iliyoathirika zaidi na faini kutokana na mashabiki wao kwani katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania mashabiki walisogea karibu na chumba cha waamuzi kisha kuwatolea lugha ya matusi na timu hiyo kutozwa faini ya jumla Sh 2.5 milioni.

Mwamuzi wa mchezo kati ya Mashujaa na Green Warriors alichezea makonde kutoka kwa wachezaji wa Green Warriors huku kocha wa timu hiyo, Uhuru Mwambungu akitajwa kuwa kiongozi na kutozwa faini Sh2 milioni huku wachezaji kila mmoja Sh500,000.

Waamuzi wa mchezo kati ya Copco na Mbuni nao walitolewa lugha ya matusi na kocha masaidizi wa Mbuni FC ambaye alitozwa faini Sh1 milioni na kufungiwa michezo nane.

Katibu wa Copco, Charles Makena anasema ugeni wa Copco umewafanya kujifunza mambo mengi sababu waamuzi wamekuwa wakiwabeba sana wenyeji ndio maana unakuta michezo mingi faini zinazotoka zinakwenda kwa wageni ambao wanakuwa hawaridhishwi na mwenendo wa mchezo, unakuta timu inalazimishiwa kushinda hata kama haikujiandaa.

MALIPO YA WAAMUZI Kutokana na uwepo wa changamoto ya udhamini wa Ligi ya Championship waamuzi hulipwa malipo ya siku (Per diem) Sh 150,000, posho (allowance) Sh 200,000 na usafiri (transport) hutegemea na umbali wa mwamuzi anapotoka.

Malipo hayo huwahusu waamuzi wote, wasimamizi wa mchezo (Match Comm) pamoja na waangalizi wa mchezo (Genaral Codinator) ambaye yeye mara nyingi hupokea posho inayoweza kufika Sh300,000.

"Match Comm anaweza kutoka nje au ndani ya mkoa inategemeana na mashindano hayo kwa mfano aliyepangwa awali alikuwa anatoka Morogoro kwenda Arusha halafu dakika za mwisho akapata tatizo hivyo shirikisho wataangalia nani yupo karibu.

"General Codinator anaweza pia kutoka sehemu yeyote sema mara nyingi huangalia yule wa ndani ya mkoa maana huyo ni kama mtunza muda kwenye mchezo na kuhakikisha utaratibu umefuatwa ili kusaidia hata zile tabia za upangaji matokeo," alisema mmoja wa viongozi soka kutoka mkoa.

"Match Comm ndio mwenye mchezo na sio sio GC (Genaral Codinator), mimi ndiye ninayekagua timu na baadaye kurudi jukwaani ambapo ndio nitaandika ripoti nzima ya mchezo.

"Hatuna mshahara maalumu bali ni nauli pamoja na 'Per diem' ambapo hutegemeana na mtu anatoka wapi hivyo utapewa kulingana na gharama ulizotumia ndio TFF inatulipa lakini posho huwa wote tunapewa sawa lakini GC analipwa na chama cha mkoa." anasema mmoja wa Match Comm.

HAPA KUNA TATIZO

Katika taarifa ya Bodi ya Ligi (TPLB), iliyotolewa Machi 9, 2023 Kocha msaidizi wa Mbuni FC, Daniel Kirai (kama ilivyoandikwa kwenye taarifa), amefungiwa michezo minane na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kufanya vurugu wakati wa mchezo.

Kocha huyo inadaiwa aliwatolea lugha ya matusi waamuzi kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu na baada ya hapo alimfuata mwamuzi kwa lengo la kumshambulia lakini alidhibitiwa.

Hata hivyo, ofisa habari wa Mbuni, Bahati Msilu anasema kocha wao anaitwa Danny Kirah na sio kama ilivyoandikwa kwenye taarifa lakini kuna vitu anaona haviko sawa kwenye ligi hasa katika michezo hii ya mwisho.

Daniel Kirai wengi wanamfahamu kama Katibu wa Gwambina ambaye naye anasema kosa kama hilo hata wao liliwahi kuwatokea baada ya taarifa kuchanganya vyeo.

"Huu mchezo upo sana maana wao wanaamini wamewahi kunifungia miezi mitatu lakini waliandika jina lingine, wao lengo lao wamfungie mratibu wa timu aliyekuwa anaitwa, Jumanne Shijja lakini wao wakaandika katibu wa timu, Jumanne Shija.

"Sasa hapo kumbuka katibu ni mimi (Karai), lakini mratibu alikuwa (Shija) mwisho wa siku hakuna aliyetumikia adhabu na kila mmoja aliendelea na majukumu yake," anasema Karia.

Kirai anasema aligoma kutumikia adhabu sabababu yeye sio Shija na Shija hakutumikia alisema yeye siyo katibu basi mambo yakaisha kimyakimya.

Kirai anasema mamlaka nayo ina shida sehemu sababu Kamati ya 72 inaletewa taarifa na ilipaswa kutumia vielelezo wakati wa kuhukumu maana bila hivyo kutatokea makosa kila siku.

"Huu ndio uzembe sababu kabla ya ligi kuanza kuna fomu inatumwa ambayo inajazwa kwa viongozi wote na majina yao lakini wakati wanajadili kwanini wasitumie hizo fomu kama vielelezo maana hapa inaonekana wanamjadili mtu ambaye hawamjui na kinachotokea unafeli kwa kutoa hukumu kwa mtu ambaye hayupo.

Chanzo: Mwanaspoti