Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacome kubaki Kigamboni amenifikirisha mambo mengi

Pacome 1 Goal Pacome kubaki Kigamboni amenifikirisha mambo mengi

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo anayeitwa Pacome Zouzoua ameliteka soka letu. Hata hivyo, kwa sasa atakuwa Kigamboni katika kambi ya Yanga. Jina lake halikufanikiwa kupenya katika orodha ya wachezaji wanaoiwakilisha Ivory Coast katika michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).

Nilitazamia hili, ingawa imeendelea kunifikirisha. Ivory Coast wana mastaa wengi wanaotamba nje ya nchi yao. Kujitokeza tu kwa jina lake katika kikosi cha awali cha Ivory Coast ni ushindi tosha kwake. Nadhani imetokana na mafanikio ya ASEC na Yanga katika soka la Afrika ndani ya hii miaka miwili.

Wakati mwingine timu za taifa zilizoendelea zikimaliza kuangalia wachezaji wanaocheza Ulaya huwa wanawageukia wachezaji wanaocheza ndani katika klabu ambazo zina mafanikio. Nadhani Pacome alibebwa na hili wakati alipoitwa katika kikosi cha awali.

Hata hivyo, baadaye maisha yanakuwa magumu kutoboa kutokana na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza Ulaya. Kinachonifikirisha ni pengo lililopo baina yao na sisi. Kwetu sisi sasa hivi Pacome angekuwa Ivory Coast akiiwakilisha Taifa Stars bila ya shida.

Lakini hapo hapo sio sisi tu. Hata kama Pacome angekuwa Mzambia basi sasa hivi angekuwa Ivory Coast kukiwakilisha kikosi cha Zambia. Zambia haina wachezaji wengi wa kigeni wanaotamba nje. Haishangazi kuona Clatous Chama anaitwa japo huwa hachezi.

Kama Chama angekuwa anatoka Ivory Coast sidhani kama angekuwa anaitwa katika kikosi cha nchi hiyo. Labda ambacho kwa kiasi fulani kingeweza kufanyika ni ‘connection’ kutoka kwa mawakala ambao wamekuwa wakifanya ujanja ujanja kama ule wa Ousmane Sakho.

Rafiki yetu Stephane Aziz Ki anabebwa na ukweli taifa la Burkina Faso halina wachezaji wengi wanaotamba Ulaya.

Lakini hapo hapo watu wanasahau kwamba Aziz Ki ni raia wa Ivory Coast aliyekimbilia Burkina Faso kwa sababu alijua asingepata nafasi ya kucheza Ivory Coast.

Rafiki yetu mwingine, Djigui Diarra huwa anapata bahati ya kuitwa katika kikosi cha Mali kwa sababu Afrika haijapeleka makipa wengi barani Ulaya na inakuwa chaguo rahisi kwa makipa wengi wa Afrika kuitwa hata katika nchi ambazo zimeendelea kisoka.

Linapokuja suala la Pacome limenifikirisha namna pengo letu na wenzetu lilivyo kubwa. Fundi kama yeye anakosekana katika kikosi chake cha timu ya taifa. Unajua ni kina nani ambao wanacheza nafasi yake?

Hapa ndipo unapoona pengo baina ya Taifa Stars na wenzetu. Hapa ndipo unapoona safari kubwa kisoka ambayo tunayo kuweza kuwafikia wenzetu katika kiwango cha kushindana. Unapomwona mchezaji kama Pacome hayupo kikosi cha Ivory Coast unahisi ugumu wa safari yetu.

Pia huwa ninawaza kuhusu vijana wetu. Vijana wetu wanadhani ni rahisi kucheza nje ya nchi. Kama Pacome yupo nchini unawezaje kuota ndoto za kucheza Ulaya bila ya kuimarisha kiwango chako maradufu.

Ni kweli wakati mwingine inatokana na ‘connection’ na mengineyo lakini kama kwa kiwango hiki Pacome yupo nchini vipi kwa viungo wetu ambao wanabweteka na kushindwa kufanya mazoezi ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha viwango vyao?

Na hapo ndipo kwa namna moja au nyingine unapolazimika kuwasifu wachezaji kama Mbwana Samatta na Novatus Dismas. Wamecheza Ulaya kwa mafanikio, ingawa kuna wachezaji wengi wa Afrika Magharibi wameshindwa na wapo barani hapa huku wengine wakiangukia kwetu.

Kitu kingine kinachonifikirisha kuhusu Pacome ni kwamba hata litakapokuja suala la wachezaji wetu kuondoka nchini na kwenda katika nchi ambazo zimeendelea kisoka basi wataendelea kuondoka hawa hawa kina Pacome.

Nafasi yao ya kuondoka Kwenda nje ni kubwa kuliko wachezaji wetu wazawa. Imetokea kwa kina Tuisila Kisinda, Chama, Fiston Mayele. Hata sasa hivi mawakala wakitazama wachezaji wa timu zetu kubwa wanaweza kutamani kuondoka na wachezaji wa kigeni zaidi kuliko wale wa ndani.

Linapokuja hitimisho la yote haya huwa nafikiria namna ambavyo hatuzalishi tena wachezaji mahiri wa ndani. Zaidi ni kuanzia nafasi ya kiungo Kwenda mbele. Vijana wa kileo hawataamini soka letu liliwahi kuwa na mastaa wengi kama Pacome au zaidi yake.

Walikuwepo kina Hamis Gaga, Nico Njohole, Steven Mussa, Athuman China, Steven Nyenge na wengineo wengi. Walikuwa zaidi ya Pacome lakini kwa sasa ni ngumu kumuaminisha kijana wa kizazi kipya kwa sababu hata kwa sasa anaona pengo kubwa lililopo kati ya kina Pacome na wachezaji wetu.

Hata ukimwambia kijana wa kileo Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alikuwa bora kuliko Mayele ni lazima utabishiwa kwa sababu hata kwa sasa hakuna mshambuliaji wa ndani anayeonyesha dalili za kumfikia Mayele.

Ukweli ni zamani walikuwepo na kama hizi pesa zetu zingekuwepo basi tungeweza kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Afrika kwa kutumia wachezaji wa ndani tu.

Zamani tulikuwa na kina hawa Pacome wengi tu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: