Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacome anajua mpaka anakera!

Pacome Zouzoua Nov.jpeg Pacome Zouzoua.

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati anatambulishwa kwa mashabiki, kuna watu walimchukulia poa. Unajua kwa nini? Hakuwa na rekodi tamu za kusisimua, zaidi ya kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.

Na hii ilichangiwa zaidi na kiburi walichokuwa nacho Wana Yanga baada ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ikiwa chini ya Nasreddine Nabi na majembe ya maana kama Fiston Mayele, Stephane Aziz KI, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Jesus Moloco na Bernard Morrison iliwapa raha Wanayanga.

Kingine ni kwamba hakuanza na moto tangu ajiunge na timu hiyo. Lakini kumbe mwamba huyo alikuwa akiusoma mchezo na kuzoea mazingira ya soka la Tanzania.

Rekodi zinaonyesha wakati anatua Yanga msimu huu, alitoka kuifungia Asec Mimosas ya Ivory Coast mabao saba na kuasisti mara nne akiwa ndiye mchezaji bora wa klabu hiyo, mbali na kuwa MVP wa ligi ya nchi hiyo, akiwa amewazidi wachezaji wenzake, Kramo Aubin aliyesajiliwa Simba na Mohamed Zoungrana aliyenyakuliwa na USM Alger ya Algeria.

MOTO UKAANZA

Kumbuka Pacome alisajiliwa na Asec msimu wa 2021-2022, akitokea African Sports ili kuziba nafasi ya Aziz KI aliyekuwa amenyakuliwa na Yanga.

Hivyo akatua Jangwani na kukutana na Aziz KI pamoja na Yao Kouassi aliyekuwa akicheza naye Asec na mambo yakawa ni moto kwani alianza kuonyesha rangi yake halisi uwanjani, kwenye mechi za raundi ya kwanza ya Ligi y Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS ya Djibouti.

Awali alionekana kama mchezaji wa kawaida kwenye mechi za Ngao ya Jamii, hasa baada ya kushindwa kukwamisha penalti wakati Yanga ikilitema taji mbele ya Simba pale Mkwakwani, Tanga.

Unalikumbuka lile bao alilomtesa kipa na mabeki wa ASAS wakati Yanga ikiifumua Wadjibouti kwa mabao 5-1. Achana na bao hilo, lakini kiumbe hicho kiliupiga mpira mwingi na kuifanya Yanga kufanya watakacho uwanjani.

Yanga ikavuka hatua hiyo n kwenda raundi ya pili, ambapo akishirikiana na wenzake waliivusha salama Yanga hadi makundi kwa mabao ya Clement Mzize aliyeifunga El Merreikh ya Sudan nje ndani.

KATIKA LIGI

Kuna waliombeza Zizzou huyo wa Ivory Coast kwamba Wadjibouti aliwaonea, lakini kile alichokifanya kwenye mechi tisa za Ligi Kuu hadi sasa kimethibitisha kuwa, jamaa ni fundi kwelikweli na jinsi anavyocheza unaweza kuhisi soka ni rahisi, kumbe ni kipaji alichoncho.

Alianza kuwanyanyasa KMC iliyoingia kwenye mfumo na kupasuliwa mabao 5-0, Pacome akifunga la mwisho kikatili, kisha akarudia tena mbele ya Ihefu kwa kufunga bao la mapema, ambalo hata hivyo halikuisaidia Yanga kuepuka kipigo cha 2-1 mbele ya Wazee Mbogo Maji.

Pacome hakuridhika na kuchachafya mabeki tu na kuwasaidia wenzake kufunga mabao, alifunga tena wakati wanaizamisha Geita Gold, aliitanguliza Yanga kisha wenzake wakaongeza mawili na Yanga kurudi kwenye wimbi la ushindi katika mechi za Ligi Kuu.

Ufundi wake na ule wa nyota wenzake wa kikosi cha Yanga uliifanya Yanga iendelee kutoa dozi, ikiizamisha Azam FC kwa mabao 3-2 katika bonge la mechi iliyokuwa ngumu na tamu kwa wakati mmoja. Zikapita jumla ya mechi mbili bila ya Pacome kufunga, lakini aliendelea kuwavuruga mabeki wa timu pinzani wakati Yanga ikivuna pointi tatu, ndipo ikafikia Novemba 5, siku ya Kariakoo Derby.

Pacome akaivuruga ngome ya Simba akishirikiana na Clement Mzize aliyetokea benchi nayo ikafa kwa mabao 5-1.

Wakati mashabiki wa Simba wakianza kutoka kwa kudhani matokeo yatasalia kuwa 4-1, Pacome akafunga mkwaju wa penalti baada ya Aziz KI kufanyiwa madhambi na Henock Inonga.

Hilo lilikuwa bao la tano kwa Yanga, lakini likiwa ni la nne kwa nyota huyo aliyeanza soka lake katika Akademi ya Sparta Prague ya Jamhuri ya Czech akianzia kikosi B mwaka 2016.

MOTO WA MAKUNDI

Pacome aliyewahi kuichezea pia timu ya SC Gagnoa y Ivory na BFC Dugavpils ya Latvia aliendelea moto wake kwenye mechi za hatua ya makundi ambapo Yanga imecheza mechi tatu, ikipoteza moja kwa mabao 3-0 ugenini mbele ya CR Belouzidad ya Algeria kisha kutoka sare mbili dhidi ya watetezi Al Ahly ya Misri na Medeama ya Ghana.

Katika mechi hizo mbili, ikianzia ile ya Al Ahly iliyopigwa Kwa Mkapa, Pacome alikuwa na kazi ya kuinusuru timu isipoteze kwa kusawazisha mabao. Wamisri walitangulia kupata bao dakika ya 87 na kufikiri biashara ilikuwa imeisha, lakini Pacome alifanya yake, Yanga ikavuna pointi moja.

Wikiendi iliyopita Yanga ilisafiri hadi Kumasi, Ghana kuvaana na Medeama, wenyeji wakatangulia kupata bao la penalti lililowekwa na Jonathan Sowah, lakini Pacome alipambana na kusawazisha na kuipa timu hiyo pointi ya pili na wikiendi hii timu hizo zitarudiana Kwa Mkapa.

Sio kufunga mabao tu, lakini Pacome amekuwa akijituma mno uwanjani kuanzia mechi ile ya ugenini dhidi ya Belouizdad hadi hizo nyingine mbili, kwani nyota kadhaa wa Yanga kama Aziz KI, Maxi Nzengeli na washambuliaji wengine walionekana kuyumba mbele ya lango la wapinzani.

NINI KITAFUATA?

Kwa aina ya uchezaji wake, imemfanya Pacome kujitofautisha na wenzake, kwani hata ukirejea kwenye pambano la Simba na Yanga, kiungo mshambuliaji huyo alikuwa akiifuata mipira nyuma kisha kukimbia nayo na kutoa pasi kwa wenzake zilizochangia timu yake kuandika historia mpya.

Kama ataendeleza na moto huo ni wazi mabeki wa timu pinzani na makipa watakuwa na kazi kubwa kutokana na ukweli Pacome ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kutoa pasi zenye macho, mbali na kufumua mashuti makali na kufunga mabao.

Kitu pekee kinachoweza kumkwamisha nyota huyo aliyezaliwa Aprili 30, 1997 katika kitongoji cha Port Bouet, Abidjan, labda ni majeraha. Ni wazi Yanga haijapoteza fedha kumsajili Pacome aliyekulia kwenye Kitongoji chenye vurugu n uhuni mwingi cha Port Bouet, kwani ni aina ya wachezaji wanaojua kuburudisha na kuipigania timu uwanjani bila kuchoka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live