Bao alilofunga na asisti mbili alizotoa kwa Clatous Chama na Pa Omar Jobe usiku wa jana wakati Simba ikiizamisha Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0 katika mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika, limemuingiza kiungo mshambuliaji wa Msimbazi, Saido Ntibazonkiza vitani dhidi ya Pacome Zouzoua wa Yanga.
Saido alifunga bao la kuongoza la Simba katika dakika ya salba tu akimegewa pande tamu na Chama wakati timu hiyo ikipata ushindi huo mnono ulioivusha kwenda robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya nne ndani ya misimu sita, kabla ya kuasisti bao la pili na nne na kumfanya ahusike kwenye mabao manne hadi sasa kwenye michuano hiyo.
Idadi hiyo ya mabao aliyohusika nayo nyota huyo wa kimataifa wa Burundi imelingana na ile aliyonayo Pacome aliyefunga mabao matatu na kuasisti moja akishika nafasi ya pili ya vinara wa mabao hadi mechi za makundi zilipomalizika usiku wa jana kwa kushuhudiwa timu nane zikitinga robo fainali huku Tanzania ikiweka rekodi kupitisha mbili.
Pacome aliyesajiliwa na Yanga msimu huu kutoka Asec Mimosas yupo nyuma ya Sankara Karamoko aliyekuwa Asec Mimosas ambaye ameuzwa hivi karibuni barani Ulaya katika timu ya Wolfsberger AC akiwa amefunga mabao manne na kuasisti moja katika hatua ya makundi na kuiwezesha timu hiyo ya Ivory Coast kufuzu mapema robo kupitia Kundi B ikiitangulia Simba.
Kwa mujibu wa orodha ya wafungaji, Saido kwa sasa anashika nafasi ya tano akiwa nyuma ya Hussein El Shahat wa Al Ahly na Abdelraouf Benguit wa CR Belouizdad wenye mabao matatu kila mmoja kama Pacome, huku Mrundi huyo akifuatiwa na Glody Likonza wa TP Mazembe, Fiston Mayele wa Pyramids na Yan Sasse wa Esperance wenye mabao mawili na asisti moja.
Saido alifunga bao la kwanza kwa njia ya penalti katika mechi dhidi ya Asec kabla ya juzi tena kuongeza, wakati Pacome ambaye amekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kwa aina ya uchezaji wake alifunga kwenye mechi dhidi ya Al Ahly na Medeama aliowatungua mara mbili nyumbani na ugenini.
Pia aliasisti dhidi ya CR Belouizdad na kushindwa kuhusika na bao kwenye mechi mbili tu, ile ya kwanza yaugenini dhidi ya CR Belouizdad ambapo Yanga ilikufa 3-0 na kwenye kipigio cha 1-0 ugenini dhidi ya Al Ahly wikiendi iliyopita.
Nyota wengine wa Simba na Yanga waliopo kwenye orodha ya wafungaji ni pamoja na Willy Onana (Simba) na Mudathir Yahya waliofunga mabao mawili kila mmoja, huku Stephane Aziz KI na Kennedy Musonda wote wa Yanga kila mmoja amefunga bao moja moja na kuasisti mabao mawili, wakati Chama na Kibu Denis wote wa Simba wakifunga moja moja na kuasisti moja moja kwenye mechi za makundi.
Nyota hao wanaochuana na wakali wengine wa klabu nyingine sita zilizopenya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, wana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao iwapo watakomaa kwenye mechi mbili za kila timu za hatua hiyo inayotarajiwa kupigwa mwishoni mwa mwezi huu mara baada ya droo kufanyika wiki ijayo.
Mbali na Simba na Yanga zilizotinga hatua hiyo zikiwa ndizo pekee kutoka nchi moja msimu huu kufuzu kwa pamoja, pia kuna mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Petro Atletico ya Angola, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Esperance ya Tunisia.
Simba ina uwezekano wa kukutana na moja kati ya Mamelodi, Petro na Al Ahly zilizomaliza kama vinara wa makundi ya A, C na D, huku Yanga ikiwa na nafasi pia ya kukutana na Mamelodi, Petro au Asec iliyoongoza Kundi B.
Msimu uliopita kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga ilitoa mfungaji bora wa michuano hiyo baada ya Mayele kufunga mabao saba akimpiku Ranga Chivaviro aliyekuwa Marumno Gallants ya Afrika Kusini aliyemaliza na sita.
Mayele aliyefunga pia mabao saba kwenye mechi za awali za CAF za msimu huo na 17 ya Ligi Kuu akiwa kinara sambamnba na Saido msimu uliopita kwa sasa yupo Pyramids, wakati Chivaviro anaipiga Kaizer Chiefs na wote wamekuwa na wakati mgumu kulinganisha walivyokuwa na timu zao za msimu uliopita.