Yanga imebakiza mabao 45 tu katika mechi 25 zilizobaki Ligi Kuu ili ifikie rekodi yake ya ufungaji ya msimu uliopita, lakini tayari imejiwekea rekodi mpya ya kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika raundi tano za mwanzo ambayo haikuwahi kuweka siku za nyuma huku mchango mkubwa ukiwa wa viungo Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz Ki.
Hadi sasa, Yanga imefumania nyavu mara 15, jambo ambalo haikuwahi kufanya, lakini shukrani za kipekee ziende kwa mastaa hao ambao wao pekee kwa pamoja wamefunga asilimia 73.3 ya mabao yote huku 26.7 yakifungwa na wenzao.
Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tano Yanga ilizocheza - kila mchezo kumekuwa na bao ambalo limefungwa na mmojawapo kati ya viungo hao, ingawa baadhi ya michezo wawili au watatu kati yao walifunga.
Nyota hao wanne wamefunga mabao 11 kati ya 15 na wameonekana kugawana vyema kwani Aziz Ki, Pacome na Nzengeli kila mmoja amepachika matatu na Mudathir mawili.
Hatari yao kufunga ilianza mechi ya kwanza dhidi ya KMC waliyoibuka na ushindi wa mabao 5-0 ambapo Aziz Ki, Pacome na Mudathir kila mmoja alifunga moja huku mawili yakipachikwa na Hafidh Konkoni na Dickson Job.
Baada ya hapo waliendeleza balaa dhidi ya JKT Tanzania ambapo walitakata kwa ushindi wa mabao 5-0 Nzengeli alifunga mawili na moja likipachikwa na Aziz Ki, huku Kennedy Musonda na Yao Atohoula wakifunga.
Mchezo uliofuata dhidi ya Namungo FC, bao pekee la ushindi liliwekwa kimiani na Mudathir na mchezo dhidi ya Ihefu waliofungwa 2-1, bao la kufutia machozi lifungwa na Pacome.
Jeuri ya viungo hao iliendelea juzi dhidi ya Geita Gold waliposhinda mabao 3-0 ambapo watatu kati yao ndio walifunga kina Nzengeli, Aziz Ki na Zouzoua.
Lakini sio tu wamekuwa na mchango kufunga bali hata kupiga pasi za mwisho ambapo Mudathir ametoa asisti mbili sawa na Nzengeli huku Azi Ki akipiga moja.
Kufanya vizuri kwa viungo hao ni kama kunatimiza maono ya kocha wa Yanga, Miguel Gamondi aliyewahi kusema anahitaji mabao yatoke kwa wachezaji wa idara tofauti uwanjani badala ya washambuliaji pekee.
“Kazi ya kufunga haipaswi kuwa kwa washambuliaji tu. Nataka kuona wachezaji wa nafasi tofauti kwenye timu yangu wanafunga mabao na sio kutegemea washambuliaji tu. Naamini wachezaji nilionao wanao uwezo wa kufanya hivyo,” alinukuliwa Gamondi.