Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacome, Kanoute waiteka Ligi Kuu Bara

Pacome Chama Pc Pacome, Kanoute waiteka Ligi Kuu Bara

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Upepo umehamia Magharibi. Miaka ya nyuma ilikuwa nadra sana kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara kushusha vyuma kutoka ukanda wa Afrika Magharibi, walishuhidiwa kwa wingi wakisajiliwa wachezaji kutoka mataifa jirani, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia na hata DR Congo.

Lakini upepo umehamia Magharibi. Miaka ya nyuma ilikuwa nadra sana kwa klabu za Ligi Kuu Bara kushusha vyuma kutoka Ukanda wa Afrika Magharibi, walishuhidiwa kwa wingi wakisajiliwa wachezaji kutoka mataifa jirani, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia na hata DR Congo.

Lakini kwa sasa wachezaji kutoka ukanda huo wamekuwa wakimiminika kwa wingi Tanzania na sio kwa ajili ya kuzichezea Simba na Yanga pekee ambazo zinafahamika ni kongwe na maarufu Afrika, pia upande wa klabu za daraja la kati kama vile Singida Big Stars na nyinginezo.

Nini kinawavuta wachezaji kutoka ukanda huo? kocha wa zamani wa Yanga, Singida BS na Azam FC, Hans van der Pluijm anaamini kupanda thamani kwa ligi ya Tanzania ni miongoni mwa mambo yaliyochochoea hilo.

“Ligi ya Tanzania inakua kwa kasi sana, ikiwa ligi ina mvuto ni rahisi wachezaji kutoka kwenye mataifa makubwa zaidi ya soka kuvutika, tumekuwa tukiona kwa miaka ya hivi karibuni namna ambavyo timu zake zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa,” anasema kocha huyo.

Kwa upande wa kocha wa timu ya vijana wa Azam FC, Mohammed Badru, anasema, “Wapo wachezaji ambao wamepita Tanzania na kuwa na hatua kubwa kwenye maisha yao ya soka mfano mzuri ni Sakho ambaye alienda Ufaransa na wengine kibao ambao walijikuta wakipata nafasi kwenye klabu nyingine kubwa zaidi.”

“Wapo wachezaji ambao wanavutika kutokana na mvuto wa ligi maana kwa sasa ligi yetu ipo kwenye zile ligi 10 bora Afrika, wengine wanakuja wakijua Tanzania kuna fursa za wao kupiga hatua,” anasema Badru.

Kulingana na ubora wa wachezaji hao kila mmoja kwenye nafasi yake hiki hapa kikosi matata cha wachezaji kutoka Afrika Magharibi wanaokiwasha Ligi Kuu Bara kiasi cha wengine kuapata nafasi hadi katika timu zao za taifa.

DJIGUI DIARRA (YANGA

Kwa miaka mingi, Aishi Manula amekuwa hana mpinzani ligi kuu, hata hivyo ujio wa Diarra umeleta mapinduzi. Ni mmoja wa makipa waliokamilika na nyota huyo kutoka Mali ameifanya Yanga kuwa imara, ni mchezaji kiongozi ambaye amekuwa akishirikiana vyema na Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambao wamekuwa wakicheza mbele yake kwenye eneo la kati huku pembeni wakiwa, Joyce Lomalisa, Kouassi Attohoula ‘Yao’ na Nickson Kibabage.

Diarra alikuwa mchezaji muhimu wakati Yanga ikiweka historia ya kucheza fainali ya kombe la Shirikisho Afrika na ilipoteza kwa kanuni dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla ya sare ya mabao 2-2.

Kama haitoshi, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kipa bora wa mwaka 2023, lakini alizidiwa kete na Yacine Bounou (Morocco, Al Hilal ya Saudi Arabia), Mohamed El-Shenawy (Misri, Al-Ahly ya Misri) na Andre Onana (Cameroon, Manchester United) ambao waliingia tatu bora.

KOUASSI ATTOHOULA (YANGA)

Kiwango cha Yao kilimfanya Kibwana Shomary ambaye alikuwa akitumika kama beki wa kulia kwenye kikosi cha Yanga kuandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba kazini kwake kuna kazi, jamaa ameonyesha ubora mkubwa tangu ajiunge na Wananchi ni kati ya sajili ambazo hazikuhitaji muda mrefu kuonyesha thamani zao.

Yao ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara, ameonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia na kushambulia ambapo hadi sasa ndiye beki aliyetoa asisti nyingi zaidi (6). Nguvu, kasi na maarifa ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimbeba mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.

CHEIKH SIDIBE (AZAM)

Azam ilimwona, Sidibe aliyekuwa akiichezea Teungueth FC ya Senegal ana uwezo wa kuvaa viatu vya Bruce Kangwa aliyeonekana umri kumtupa mkono.

Sidibe ambaye ni beki wa kushoto anaendelea kutuonyesha mabosi wa Azam FC hawakufanya makosa kumsajili, amekuwa akionyesha ubora wa mkubwa katika kushambulia na kuzuia kwenye kikosi cha Youssoph Dabo.

DANIEL AMOAH (AZAM)

Tangu kutundika daruga kwa Aggrey Morris, Daniel Amoah amekuwa muhimili wa idara ya ulinzi ya Azam FC na ndiye nahodha wa kikosi hicho.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ghana kwa sasa anaonekana kuzoea ligi ya Tanzania, utimamu wake wa mwili umekuwa ukimsaidia kupigana vikumbo na washambuliaji mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye ligi.

MALICKOU NDOYE (AZAM FC)

Majeraha ndio yaliyomfanya kukaa nje ya uwanja kwa sasa, ni beki mwenye uwezo mzuri wa matumizi ya nguvu na akili, kama angekuwa fiti ni wazi kuwa pengine Azam FC isingeingia sokoni katika dirisha dogo lililopita la usajili na kushusha beki mwingine wa kati kwa ajili ya kuimarisha eneo hilo.

Msenegal huyo wakati atakaporejea atakuwa na kibarua cha kupigania namba mbele ya Yeison Fuentes ambaye amekuwa akipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC tangu asajiliwe kutoka Amerika ya Kusini.

SADIO KANOUTE (SIMBA)

Ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba hasa anapokuwa kwenye ubora wake, ana uwezo mzuri wa kuifanya timu kuwa na utulivu kwenye eneo la kiungo cha chini.

Akiwa uwanjani huwa hacheki na mtu kupata kadi kwake ni jambo la kawaida kutokana na staili yake ya uchezaji, sio aina ya mchezaji ambaye anaweza kuruhusu mshambuliaji ampite kirahisi kwa sasa kwenye kikosi cha Simba amekuwa akitumika juu ya Boubacar Sarr na Fabrice Ngoma.

KIPRE JR (AZAM)

Ni miongoni mwa washambuliaji wenye kasi zaidi Ligi Kuu Bara, mabeki wengi huwa hawapendi kukutana naye tena anapokuwa kwenye ubora wake, anakuwa kama kambale huwa anateleza tu kwenye iwe winga ya kulia au kushoto.

Kama gari kwa sasa ndio limewaka kwa nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast, akaunti yake msimu huu inamabao manne kwenye ligi. Hakuuanza vizuri msimu ni kama alionekana kupotea baada ya kupoteza nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza lakini kwa sasa anaonekana kuibuka upya.

PACOME ZOUZOUA (YANGA)

Wapo mashabiki ambao walitamani kumwona kiungo huyo fundi akiwa sehemu ya kikosi cha taifa lake la Ivory Coast kwenye fainali za Mataifa ya Afrika lakini kwa bahati mbaya hakuitwa kwenye kikosi cha Jean-Louis Gasset ambaye siku chache zilizopita alifutwa kazi kufuatia matokeo mabaya ya timu hiyo.

Pacome kama kuonyesha kiwango kizuri ameonyesha msimu huu na sio kwenye mashindano ya ndani tu hadi upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo alifunga mabao matatu ‘muhimu’ ambayo yameifanya Yanga kuwa na matumaini makubwa ya kuvuka hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Licha ya msimu wake wa kwanza kwenye ligi, fundi huyo ameifungia Yanga mabao tisa, kijumla katika mashindano yote.

ALASSANE DIAO (AZAM)

Alipotua Azam wadau wengi wa soka nchini walikuwa wakimbeza lakini kwa sasa anatajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji hatari, anabebwa na ukubwa wa umbo lake pamoja na kasi, anaweza kutumika katika maeneo yote ya ushambuliaji japo mwenye amekuwa akifurahia zaidi kucheza namba tisa.

Hivi karibuni Diao amekuwa rafiki wa nyavu na aliibeba Azam FC kwenye Michuano ya Kombe la Mapindizi kwa kupachika mabao manne.

STEPHANE AZIZ (YANGA)

Ndiye mchezaji hatari zaidi wa kigeni kwenye ligi. Ndiye kinara wa kufunga bara akiwa na mabao 10.

Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Azizi Ki kutokana na panda shuka ya kiwango chake lakini hata hivyo alikuwa sehemu ya wachezaji muhimu ambao waliifanya Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa kiwango ambacho anakionyesha Azizi ni wazi viongozi wa Yanga watakuwa na wakati mgumu kuhakikisha fundi huyo anaendelea kusalia Jangwani kwani tayari klabu kubwa zaidi Afrika zimeanza kuvutiwa naye.

MAROUF TCHAKEI (IHEFU)

Alianza maisha akiwa na Singida Fountain Gate msimu huu na kufunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara kisha Januari mwaka huu akajiunga na Ihefu na hadi sasa amefunga matatu na kumfanya kufikisha idadi ya mabao manane akiwa na kikosi hicho.

Wengine; Augustine Okrah (Ghana, Yanga), Pa Omar Jobe (Gambia, Simba), Joseph Guede (Ivory Coast, Yanga), Freddy Michael (Ivory Coast, Simba), James Akaminko (Ghana, Azam), Christian Zigah (Ghana, Dodoma Jiji), Djibrill Sylla (Gambia, Azam), Morice Chuku (Nigeria, Singida FG), Enock Atta Agyei (Ghana, Singida FG) na Nicholas Gyan (Ghana, Singida FG).

KOCHA: Youssoph Dabo (Azam)

AFRIKA MAGHARIBI

Benin (0)

Burkina Faso (1)

-Azizi KI

Gambia (2)

-Djibrill Sylla, Pa Omar Jobe

Ghana (6)

-Augustine Okrah, James Akaminko, Daniel Amoah, Christian Zigah, Enock Atta Agyei, Nicholas Gyan

Guinea-Bissau (0)

Guinea (0)

Ivory Coast (5)

-Joseph Guede,Pacome Zouzoua, Kipre Junior, Kouassi Attohoula Yao, Freddy Michael

Liberia (0)

Mali (2)

-Djigui Diarra, Sadio Kanoute

Mauritania (0)

Nigeria (1)

-Morice Chuku, Emotan Cletus, John Noble

Niger (0)

Senegal (3)

-Alassane Diao, Cheikh Sidibe,Malickou Ndoye

Sierra Leone (0)

Togo (1)

-Marouf Tchakei.

Chanzo: Mwanaspoti