Mashabiki wa Yanga wanaendelea kuchekelea baada ya kushuhudia timu hiyo ikianza Ligi Kuu kwa kishindo ikiifumua KMC mabao 5-0, lakini sifa zikienda eneo la kiungo kutokana na Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI walifanya balaa kubwa.
Yanga ilipata ushindi huo wa kwanza mkubwa katika historia baina ya timu hizo mbili ambapo kabla haikuwahi kushinda zaidi ya mabao mawili kwenye mechi 10 zilizopita, lakini ikaelezwa kilichoiua KMC ni mtego uliosukwa kupitia eneo la kiungo lililotawaliwa na Pacome na Aziz KI. Ubora wa eneo lao la kiungo likiwahusisha viungo watano akiwamo viungo wabakaji wawili Khalid Aucho na Mudathir Yahya.
Aucho alikuwa na jukumu la kuhakikisha hasogei sana juu na kuacha wazi eneo la mbele ya mabeki wao wa kati kazi ambayo ameonekana kuifanya kikamilifu, huku Mudathir ambaye mbali na kukaba kwa nguvu sawa na Mganda huyo lakini alikuwa na kazi nyingine ya kuongeza idadi kwa viungo wengine wawili wa juu hasa timu inaposhambulia.
Viungo hao wa juu kulikuwa na Aziz KI na Pacome ambao licha ya kuwa viungo washambuliaji wa aina moja ndio walikuwa mwiba kwa viungo wa timu pinzani.
Aziz KI alikuwa muda mwingi anacheza huru akionekana kama winga, lakini akitumia muda mwingi kusogea kati akipishana na Pacome ambao ufundi miguuni wanapokuwa na mipira uliwafanya viungo na mabeki wa KMC kutawanyika na kutengeneza eneo la kati kuwa wazi kwa Yanga kuleta madhara.
Pasi za Aziz KI na Pacome ziliifanya KMC kuonekana wa kawaida wakitumia vyema falsafa ya soka la kocha wao Miguel Gamondi ambaye tangu ametua Yanga ameonekana hataki kuona mchezaji anakaa na mpira kwa zaidi ya sekunde mbili mguuni.
Pembeni ya viungo hao wawili wa juu kulikuwa na kiungo mwingine wa pembeni mshambuliaji Jesus Moloko ambaye mbali na kuwa na kazi ya kukimbiza kutokea pembeni kulia, lakini alitengeneza idadi ya kutosha pale ambapo Yanga ilipoteza mpira kwa kuja chini kusaidia kupokonya mipira.
UKUTA UMETULIA
Ubora wa wa eneo hilo la kiungo ulipunguza presha kubwa kwa mabeki wao wa kati na hatimaye kipa wao ambapo falsafa za Gamondi zilionekana kuwapa wakati mgumu wapinzani kupiga pasi zaidi ya tano eneo la Yanga kutokana na mabingwa hao sasa kuonekana wakifika haraka kwa wapinzani wakiwalazimisha kuachia mipira kwa haraka lengo ambalo lilitimia.
MSIKIE GAMONDI
Akizungumzia soka hilo Gamondi licha ya kuwapongeza wachezaji wake mabeki na viungo kwa kucheza kwa ubora mkubwa lakini alitoa kauli akionyesha kuhitaji mabao zaidi kutokana na wingi wa nafasi wanazozitengeneza.
“Vijana walicheza kwa ubora mkubwa kuanzia nyuma na eneo la kiungo tulionekana kutulia na kuwabana vizuri wapinzani wetu, tunawaheshimu sana wapinzani wetu ni timu nzuri lakini nadhani tulistahili ushindi mkubwa zaidi ya huu,” alisema Gamondi.
“Tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga kwa mfano mzuri kipindi cha kwanza ambacho hatukutulia kutumia nafasi nyingi tutaendelea kuhimizana kuongeza umakini, jambo zuri tunaona viungo, washambuliaji na hata mabeki wanafunga hii itawoangezea hali ya kujiamini kwenye mechi zijazo.
Staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekero’ alisema ; ““Nadhani kutulia kwao kunatokana na safu ya kiungo, sawa ni mechi chache lakini kuna kitu kikubwa kocha amefanikiwa kutengeneza uwiano mzuri wa viungo ambao anawatumia. Yanga ina safu bora ya kiungo kwasasa wanaonekana kucheza kwa mbinu nyingi nadhani kitu ambacho kimesalia ni kocha kuongeza utulivu kwa washambuliaji wake ili wafunge zaidi.”