Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacome, Aziz Ki walamba Sh400M

Aziz KI X Pacome Pacome, Aziz Ki walamba Sh400M

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Yanga bado wako kwenye sherehe ya ushindi mkubwa dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na mchezo mmoja mkononi, lakini kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi amesema kazi haijaisha, huku mastaa wa timu hiyo wakivuna Sh400 milioni za ushindi huo wa kibabe.

Yanga imesaliwa na mechi mechi dhidi ya vinara wa sasa wa kundi D na watetezi wa taji, Al Ahly ya Misri mechi itakayopigwa Ijumaa hii na kocha Gamondi ameweka wazi kuwa ‘haijaisha hadi iishe’ wakitaka ushindi ugenini kusudi aongoze kundi hilo ili iwe na kazi rahisi kwenye robo fainali ambayo droo yake inatarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema amefurahia timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Belouizdad lakini hapo hapo bado anafikiria kwenda Misri kuwafuata Al Ahly akitaka kusaka ushindi.

Gamondi alisema anajua kuna faida kubwa, Yanga ikimaliza kinara wa Kundi D ambapo haitakuwa na ugumu mkubwa kuelekea droo ya nani wakutane naye kwenye hatua ya robo fainali, lakini akiwakumbusha mastaa wake kuwa makini kuzitumia nafasi inazotengeneza ili kupata mabao mengi, kwani hata juzi ilistahili kushinda kwa idadi kubwa zaidi.

“Kwangu hatua ya kufuzu kwenda robo fainali nimeridhika, lakini ukweli ni kwamba kuna faida kubwa kama tukimaliza vinara wa kundi letu mbele ya Al Ahly. Safu ya ushambuliaji ina udhaifu, inatengeneza nafasi nyingi inatumia chache pia eneo la ulinzi kuna makosa madogo madogo nikifanikiwa kurekebisha na wakinielewa Yanga itakuwa timu bora Afrika kwa ushindani,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Mimi ni kocha ninayependa kushinda wakati wote, kila mtu anajua namna ambavyo tulipambana na Ahly hapa, ni klabu kubwa na bora lakini kila kitu kinawezekana tutakwenda kujaribu kwenda kucheza kwa akili kubwa tutafute ushindi hukohuko kwao (Ahly).”

PACOME, AZIZ KI Matokeo ya juzi katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam yamewapa nyota wa timu hiyo wakiongozwa na aliyekuwa na shughuli yake, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Djigui Diarra na Mudathir Yahya zaidi ya Sh 400 milioni kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo.

Ipo hivi. Kabla ya mchezo huo mabosi wa Yanga wakiongozwa na mfadhili wao Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ walifanya kikao flani cha mtego wa mamilioni kwa wachezaji wao. Mtego wenyewe ulikuwa hivi mabosi wa Yanga waliwaambia wachezaji wao kwamba kama wakishinda bao moja hadi mawili, basi wangevuna Sh100 milioni pekee, lakini kama ingeshinda mabao 3-0 basi dau lingeongezeka hadi Sh200 milioni, lakini kama itavuka malengo kwa kushinda mabao 4-0 watajihakikishia Sh400 milioni kwa ushindi huo.

Kama uliona juzi wachezaji wa Yanga walipofunga bao la nne tu wale waliokuwa benchi na hata wale baadhi ya waliokuwa uwanjani walionyesha vidole vinne eneo la Jukwaa Kuu wakiwakumbusha viongozi wao kwamba nne zimetimia.

Mbali na fedha hizo, Yanga imevuna Sh20 milioni kutoka kwenye ahadi ya Rais Samia Hassan.

Pia Yanga imevuna Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.3 bilioni) za CAF kwa kutinga robo fainali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: