Pamoja na stori kibao zinazoendelea kuhusiana na majeruhi wa Yanga, Mwanaspoti linajua Pacome Zouzoua na Khalid Aucho watakiwasha dhidi ya Mamelodi Sundowns Kwa Mkapa.
Lakini Yao Kouassi ni uhakika kwamba jukwaa linamhusu kwenye michezo yote miwili ule wa nyumbani na ugenini kwani atakaa nje kwa uchache wiki tatu.
Yanga itaikaribisha Mamelodi Machi 30 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana nayo wiki moja baadaye mjini Pretoria, Afrika Kusini na mshindi wa matokeo ya jumla atatinga nusu fainali kuvaana na kati ya Esperance ya Tunisia au Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Mashabiki wana presha baada ya wachezaji watano wa timu hiyo kuelezwa kuwa majeruhi, wakiwamo viungo Khalid Aucho, Zawadi Mauya na Pacome Zouzoua na mabeki wawili wa kulia, Kibwana Shomary na Yao Kouassi.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe alisema Aucho, Mauya na Kibwana hali zao zinaendelea vyema, wakati Yao mambo bado na kwa Pacome walikuwa wanasubiri ripoti kutoka kwa madaktari wa timu ya taifa ya Ivory Coast waliopo kambini Ufaransa.
“Kibwana aliyeumia kifundo anaendelea vyema, kwani kwa mujibu wa taarifa ya daktari Jumatatu ataanza mazoezi mepesi kabla ya baadaye kuungana na wenzake, Mauya hali yake imetengamaa na muda wowote ataungana na wenzake, wakati Aucho anaingia awamu ya pili ya mazoezi,” alisema Kamwe na kuongeza;
“Yao aliyepata tatizo la nyama hadi sasa hali yake ni hamsini kwa hamsini kwa ajili ya mechi hiyo ya Mamelodi, lakini kwa Pacome aliumia goti na uzuri ameitwa timu ya taifa ya Ivory Coast na tunasubiri jopo la madaktari wao kutuelezea atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani.”
Hata hivyo, taarifa za ndani ya benchi la ufundi la Yanga zimelithibitishia Mwanaspoti kwamba, Pacome jeraha lake ni dogo ndio maana ameenda kambi ya timu ya taifa na kuna uwezekano mkubwa wa kuiwahi Mamelodi, isipokuwa kwa Yao hali ni tete kwani jeraha alilopata litamuweka nje wiki tatu na ushee.
“Yao jeraha lake la kuchanika nyama za paja, litamweka nje kuanzia wiki tatu, lakini kwa Pacome hadi anaenda Ufaransa maana yake hali sio mbaya sana, hivyo tuna imani anaweza kucheza,” kilisema chanzo cha uhakika ndani ya kambi ya Yanga.
“Pacome yupo sawa na anaendelea na mazoezi na timu yake ya taifa, kama mchezaji wetu tunawasiliana naye mara kwa mara kujua maendeleo yake. Ni kweli katika mchezo na Azam aliumia, ila sio kwa ukubwa wa kumuweka nje, angekuwa na majeraha makubwa asingeweza kusafiri kwenda Ufaransa kujiunga na timu yake ya taifa,” Mwanaspoti limethibitishiwa.
Kuhusu Aucho alisema anaendelea kwa sasa na mazoezi mepesi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti aliloumia kwenye mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly tofauti na ilivyokadiriwa hapo awali na ana matumaini ya kuwahi mchezo huo muhimu wa nyumbani wa CAF.
Kamwe alieleza hali za majeruhi alisema Aucho anaendelea vyema na kwamba mashabiki wajiandae kupata burudani katikia mechi ya nyumbani itakayopigwa kuanzia saa 3:00 usiku ambayo mashabiki wanaoingia majukwaa ya mzunguko hawatalipa kiingilio chochote, kwani ni bure.
Yanga ilitinga hatua ya robo fainali ikishika nafasi ya pili katika mechi za makundi iliyotinga baada ya kupita miaka 25 tangu ilipocheza mara ya kwanza mwaka 1998, safari hii ikiwa Kundi D pamoja na Al Ahly iliyomaliza kama kinara, CR Belouizdad iliyokuwa ya tatu na Medeama ya Ghana iliyoshika mkia.
Yanga na Mamelodi zinazokuta kwa mara ya pili baada ya mwaka 2001 kupepetana katika raundi ya pili ya michuano hiyo ya Afrika na Wasauzi kushinda mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 3-2 kisha kutoka sare ya 3-3 ugenini na kuing’oa Yanga iliyokuwa chini ya Boniface Mkwasa, itapigwa Machi 30.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi anaendelea kuwapa mbinu mastaa wa timu hiyo kwa kutambua ugumu wa mchezo huo dhidi ya Mabingwa wa African Football League (AFL), licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji waliotwa timu za taifa zinazocheza mechi za kimataifa za kalenda ya FIFA.
Mastaa wa Yanga waliopo timu za taifa ni Clement Mzize, Abuutwalib Mshery, Ibrahim Bacca, Bakar Mwamnyeto na Mudathir Yahya (Tanzania), kipa Diarra Djigui (Mali), Kennedy Musonda (Zambia), Stephane Aziz KI (Burkina Faso) na Pacome (Ivory Coast).