Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pacha wa Tuisila anukia Yanga

Tuisila Pc Data Pacha wa Tuisila anukia Yanga

Mon, 5 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga msimu huu wana jambo lao, kwani licha ya kujipanga kwenye Ligi Kuu, pia inapiga hesabu za maboresho ya kikosi chao cha sasa kwa kuanza hesabu ndefu za kumchomoa winga wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’.

Nado anamaliza mkataba wake na Azam mwisho wa msimu huu na Yanga imeanza kumpigia hesabu ikitaka kusahihisha makosa yake katika kuwania saini ya winga huyo anayejua kufunga pia.

Hesabu za Yanga ni kwa sasa wana winga mmoja tu hatari Mkongomani Tuisila Kisinda na kama akikosekana basi hakuna mtu wa maana anaweza haraka kuziba nafasi yake.

Taarifa za uhakika Mwanaspoti ilizozipata ni Yanga tayari wako katika mazungumzo na mwakilishi wa winga huyo aliyeibuliwa mchangani na Mbeya City kabla ya kuwavutia mabosi wa Azam anayewabeba kwa sasa katika Ligi Kuu ikitaka kumpa mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, mtihani mkubwa kwa Yanga ni hatua ya Azam wenyewe kuingia katika mazungumzo na winga huyo kufuatia kocha George Lwandamina kumtaka Nado asalie zaidi katika timu yake ya msimu ujao.

“Tunapambana naye tuweze kumchukua wakati huu, shida naona kama yeye na meneja wake wanaongea na sisi huku wanaongea pia na Azam, ila hatutakata tamaa,” alisema mmoja wa vigogo wa Yanga ambaye yumo ndani ya kamati ya usajili (jina tunalo) aliyeongeza kwa kusema:

“Tukimpata Nado itakuwa safi kwa kuwa tutakuwa tumelinda nafasi ya wachezaji wa kigeni kwa kuwa na mtu wa maana kutoka ndani, unajua msimu huu Nado amekuwa na kiwango bora sana tunachopenda sio mtu wa kukata tamaa.”

Usajili huo wa Nado kwenda Yanga endapo utakamilika unaweza kuwa kitu muhimu katika ujio wa kocha wao mpya Sebastian Migne ambaye amekuwa akihusudu kuwa na winga zaidi ya mmoja katika timu yake.

Msimu huu Nado amekuwa staa muhimu Azam akifungia jumla ya mabao 7 akishika nafasi ya nne katika msimamo wa ufungaji unaongozwa na nahodha wa Simba na staa wa zamani wa Azam John Bocco, huku pia akiwa mmoja ya wachezaji tegemeo wa Taifa Stars.

Nado alipotafutwa na Mwanaspoti alikiri ni kweli jambo hilo lipo, lakini hawezi kulizungumzia kwani lipo chini ya meneja wake, aliyetaka atafutwe.

“Sitaki kuchanganya mambo, ndio maana nimeliacha jukumu hilo kwa meneja wangu, yeye ndiye mwenye nafasi ya kulizungumzia kwa undani, lakini sio Yanga tu, hata Azam nao wapo kwenye mazungumzo baada ya kuonesha nia ya kutaka kunibakisha kikosini,” alisema Nado.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz