Mnyama leo anashuka kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam majira ya saa 1:00 usiku kuikabili JKT Tanzania, katika mchezo wa raundi ya tatu wa Kombe la Azam la Shirikisho (ASFC).
Simba ambao wanashikilia rekodi ya kubeba taji hilo mara tatu, wanapewa nafasi kubwa ya kuvuka kutokana na kikosi chao kuwa na mabadiliko makubwa tangu kuwa chini ya kocha mpya, Pablo Franco.
Matokea ya suluhu dhidi ya watani wao Yanga Jumamosi iliyopita, yanaweza kuwa chachu kwa wachezaji wa Simba kuwaongezea ari ya kucheza kwa kujituma zaidi ili kushinda mchezo huo ambao huenda ukawa na ushindani kutokana na rekodi za timu hizo zinapokutana ingawa JKT wapo Championiship.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema maandalizi kuelekea mchezo huo ni mazuri na wapo tayari kuwakabili maafande hao. “Tangu tumemaliza mechi na Yanga tumeendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo huu na mingine ya ligi, najua JKT Tanzania ni timu nzuri hata kama wapo Championship lakini hatutawadharau tutacheza kwa nguvu ili kupata ushindi utakaotupeleka hatua inayofuata,” alisema.
Meneja huyo alisema amezungumza na kocha wao, Pablo na amemwambia katika mchezo huo kikosi chake kitakuwa na mabadiliko ya wachezaji tofauti na kile kilichocheza dhidi ya Yanga ambapo kuna wengine atawapumzisha. Alisema hiyo ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa kila mchezaji kutoa mchango wake ikizingatiwa wanakabiliwa na mashindano mengi ikiwamo ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo kwa sasa wapo kwenye hatua ya makundi.
Kwa upande wa maafande wa JKT Tanzania, Kocha Mohamed Baresi alisema anajua wanakwenda kukutana na timu kubwa na bora, lakini hilo haliwatishi kwani wamejipanga kupambana na kupata ushindi. Alisema wachezaji wake wote wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo leo na ameahidi kuwashangaza wengi kutokana na kile ambacho wamekusudia kukifanya kwenye mchezo huo.
“JKT Tanzania tumecheza na Simba mara nyingi kwa hiyo sioni kitu kigeni, tunawajua Simba nadhani wao ndio hawatujui, tumepanga kuwashangaza watu kwa kuwatoa mabingwa watetezi mapema kwenye michuano ya mwaka huu na siyo kuwakamia bali uwezo tulionao,” alisema Baresi.