Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pablo atuma salamu.. aanza na dozi ya tatu huko

Wavuni Kibu Kibu Denis akiweka mpira wavuni

Fri, 19 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu bara, Simba SC imeendeleza ubabe mbele ya maafande wa Ruvu Shooting baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Simba ambayo iliuanza mchezo huo kwa kasi ya juu na kukaba kwa nguvu ilipata mabao yake matatu katika dakika 45 za kipindi cha kwanza yakifungwa na Meddie Kagere na Kibu Denis huku Ruvu wakifunga bao pekee kupitia kwa Elias Maguli.

Simba waliandika bao la kwanza katika dakika ya 17 likifungwa na Meddie Kagere aliyeunganisha vyema kona iliyochongwa na Bernad Morrison.

Kagere alipachika bao la pili mnamo dakika ya 36 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mohamed Makaka aliyeokoa Shuti la Kibu Denis, huku bao la tatu likifungwa na Kibu Denis aliyemalizia krosi iliyopigwa na Shomari Kapombe.

Mabao hayo mawili yanamfanya Kagere kufikisha manne akiongoza orodha ya wafungaji kwenye Ligi Kuu akiwa na idadi sawa na Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania.

Ruvu Shooting walipata bao la kufutia machozi mnamo dakika ya 70 likifungwa na Elias Maguli aliyetumia vyema makosa ya walinzi wa Simba waliofanya makosa kuondoa mpira uliokuwa unazagaa langoni mwao.

Bao hilo linaharibu rekodi ya Manula ya kucheza mechi tano bila kuruhusu bao, ambapo kabla ya hapo alikuwa amecheza mechi tano sawa na dakika 450 bila kuruhusu bao.

Hata hivyo Simba walikosa mkwaju wa penalti katika dakika ya 72 ukipigwa na Erasto Nyoni lakini kipa wa Ruvu Shooting Mohamed Makaka aliuokoa.

Ushindi huo wa mabao matatu unaendeleza rekodi ya Simba mbele ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana Juni 3 mwaka huu Simba wakishinda kwa mabao 3-0.

Simba wanafikisha pointi 14 wakikamata nafasi ya pili nyuma ya vinara yenye wenye pointi 15 wakiwasikilizia kesho watakapokutana na Namungo katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz