Nyota wa Simba leo Jumapili wanarudi kambini kutoka mapumziko mafupi, ili kujiandaa na mchezo wao wa mwisho wa Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya USGN ya Niger, huku kocha Pablo Franco akiwapiga mkwara mastaa hao.
Wachezaji wa Simba hasa wasiokuwa timu za taifa walipewa mapumziko mafupi ya siku tano tangu warejee kutoka Benin walipofumuliwa mabao 3-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast na kesho wametakiwa kurudi, huku wakihitajika kuwa fiti kama walivyoondoka.
Mapema kabla ya mapumziko, Kocha Pablo aliwaeleza wasiokuwa katika majukumu ya timu ya taifa wanatakiwa kulinda utimamu wa miili kama walivyoachana mara ya mwisho maana mziki wanaokwenda kuuanza sio masihara.
Pablo aliwasisitiza wachezaji wake kila mmoja atambue umuhimu wa mechi ya USGN na hatakuwa tayari kuona wameanza mazoezi kuanzia kesho kuna wachezaji wamerudi wakiwa wameporomoka ubora wao kutokana na starehe au jambo lingine lolote lile.
Wakati anatoa mapumziko hayo siku waliyorejea nchini kutokea Benin alisema; “Tulikuwa na ratiba ngumu ya kucheza mechi mfululizo kila baada ya siku chache, kuna nyakati tulikuwa tunatumia zaidi ya saa 24 kusafiri hivyo walichoka kweli ndio maana niliwapa muda huo wa kumpumzika.”
“Baada ya kurejea kambini tutakuwa na siku saba za kufanya maandalizi tutafanya mengi ya kutosha, wachezaji itakuwa rahisi kushika vile benchi la ufundi linawapatia kwani watakuwa na hamu ya kucheza mpira baada ya kuwa na mapumziko hayo,” alisema Pablo jambo ambalo baadhi ya mastaa wameunga mkono.
Mshambuliaji Chris Mugalu alisema katika kuhakikisha analinda utimamu wake wa mwili kama walivyopewa maagizo na kocha wao amekuwa akifanya mazoezi yake binafsi.
“Nyumbani kwangu kuna vifaa vya kufanya mazoezi ya kulinda utimamu wangu wa mwili na nimekuwa nikifanya kwa siku mara mbili asubuhi na jioni. Mazoezi hayo binafsi yamekuwa yakinisaidia kuongeza ufiti wangu kwani nilikuwa na majeraha yaliyoniweka nje na kushindwa kucheza mechi,” alisema Mugalu.
Aishi Manula alisema wao waliyokuwa kambi ya timu ya taifa si tatizo kwao kwani wanaendelea na programu ya mazoezi mbalimbali kwahiyo utimamu wa miili hautapotea.
“Tukimaliza tu kambi ya Taifa Stars hatutakuwa na muda wa kupumzika siku hiyo hiyo tutaunga moja kwa moja kuungana na wenzetu wa Simba kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa USGN ambao kiukweli tumepania kupata ushindi,” alisema Manula.
Rally Bwalya alisema siku mbili za mwanzo alipumzika na muda mwingi alitumia kulala ila baada ya hapo aliendelea na programu ya mazoezi kwenye moja ya gym iliyopo karibu na anapoishi.
“Tunaenda kucheza mechi ngumu na yenye ushindani kwahiyo lazima kupata muda wa kujiandaa vya kutosha ndio maana wakati huu nafanya mazoezi haya ya nguvu ili tukiungana kwa pamoja na wenzangu kuendeleza tu kile ninachofanya wakati huu,” alisema Bwalya.
Simba watacheza mechi ya mwisho hatua ya makundi dhidi ya USGN, Aprili 3 Uwanja wa Benjamin Mkapa na wanahitaji ushindi ili kuwa na uhakika wa kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.