UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Bernard Morrison bado hajasaini mkataba mpya kikosini hapo, huku wakisema wanasubiri ripoti ya Kocha Mkuu, Pablo Franco mwishoni mwa msimu kuona kama atamuhitaji.
Mkataba wa Morrison ndani ya Simba unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa na taarifa kwamba Yanga inataka kumrudisha kikosini kwao msimu ujao.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally, alisema: “Morrison bado hajapewa mkataba mpya huku mkataba wake ukiwa ukingoni.
“Lakini hili ni suala la benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Pablo ambapo tunasubiri ripoti ya mwisho kutoka kwake kuona kama atamuhitaji basi ataongezewa mkataba wa kuendelea kusalia ndani ya timu.
“Kwa sasa Morrison bado ni mchezaji halali wa Simba na ataendelea kuitumikia timu mpaka hatima yake itakapofahamika mwishoni mwa msimu huu.”
Morrison alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu wa 2020/21 akisaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba wa miezi sita ndani ya Yanga aliyoitumikia kuanzia Januari 2020.