Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pa Jobe: Simba nipeni muda, mtaona moto wangu

Jobe Simbaa (15).jpeg Pa Jobe

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji mpya wa Simba, Pa Omary Jobe amekiri ana mtihani mgumu kutokana na kubeba matumaini ya mashabiki wa timu hiyo, lakini akawatuliza kwa kuwaambia wampe muda aendelee kuzoea kwanza mazingira kabla ya kuanza mambo.

Nyota huyo kutoka Gambia, amesajiliwa na Simba kupitia dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu sambamba na Freddy Michael Kouablan ili kuziba pengo la Jean Baleke na Moses Phiri na tayari ameshatumika kwa dakika 53 na kufunga bao moja katika mechi ya 64 Bora ya ASFC dhidi ya Tembo FC ambako alianza kikosi cha kwanza.

Pa Jobe alicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara juzi akiingia kutoka benchi katika dakika ya 82, wakati Simba ilipoifunga Mashujaa bao 1-0.

Akizungumza nasi, nyota huyo alisema amefurahi kuwepo kwenye timu hiyo na kukiri anajua mtihani unaomkabili sasa ni mkubwa, lakini amewaomba mashabiki wampe muda kwanza.

Mchezaji huyo alisema anafurahi kuona kocha wa Simba anamuamini na kumpa nafasi katika michezo yote miwili tangu ajiunge na timu hiyo, lakini ni ngumu mambo kuwa mepesi haraka.

"Simba ina viungo wazuri na mabeki wazuri wa pembeni wenye ubunifu na kama nitazoeana nao haraka basi najipanga kuwa na mwendo mzuri wa kufunga. Nina shauku kubwa ya kujua ubora wa ligi kwa maana ya timu pinzani na ushindani ulivyo ili nifahamu jinsi ya kujipanga kwenye mechi hizo, lakini nawaomba mashabiki wanipe muda,"  alisema Pa Jobe anayefahamika pia kwa jina la utani la Drogba.

Staa huyo aliyeacha rekodi Senegal ya kuwa Mfungaji Bora kipindi akicheza pamoja na kiungo wa sasa wa Simba, Babacar Sarr kabla ya kwenda Ulaya ana kazi ya kujihakikishia namba mbele ya nyota wengine wa timu hiyo akiwamo Freddy, Kibu Denis na John Bocco katika eneo hilo la ushambuliaji.

Mapema kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha aliwazungumzia wachezaji wake wapya na kusema hana hofu nao kwani wote wanaonekana wana uwezo.

Kikosi cha Simba kinajiandaa kuvaana na Tabora United katika mechi nyingine ya kiporo itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kabla ya kuhamia Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuikaribisha Azam FC katika mechi ya Mzizima Dabi itakayopigwa Februari 9.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live