Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris St-Germain inapambana kuhakikisha inaipata saini ya kiungo wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Joshua Kimmich, katika dirisha hili kwa ajili ya kuboresha eneo lao la kiungo linaloonekana kuwa vibaya msimu huu.
Kimmich mwenye umri wa miaka 28, amekuwa akitajwa kuwa kwenye rada za timu nyingi kutokana na kiwango alichoonyesha na hali ya mkataba wake wa sasa ambao unamalizika mwaka 2025, hivyo Munich isipomuuza katika dirisha hili la uhamisho au mwisho wa msimu huenda ikamuuza kwa pesa kiduchu Januari mwakani (2025) ama akaondoka bure mwisho wa msimu ujao.
Staa huyu wa kimataifa wa Ujerumani huduma yake imekuwa ikiwindwa na timu nyingi Barani Ulaya ikiwa pamoja na Liverpool na FC Barcelona ingawa Munich ndio inaonekana kukwamisha dili lake kwani inahitaji zaidi ya Pauni 50 milioni.
Timu nyingi zinaona ni hasara kulipa kiasi hicho cha pesa kwa mchezaji ambaye mkataba wake unaenda kumalizika.
Hata hivyo, ushindani unaoongezeka kwa timu zinazomhitaji kuendelea kujitokeza, huenda ukasababisha timu mojawapo kulipa pesa hiyo inayotakiwa na Bayern na kumchukua fasta kutokana na kuhofia kupigwa bao na nyingine.