Wikiendi iliyopita Ligue 1 kule nchini Ufaransa iliendelea kuuwasha moto na moja kati ya mechi zilizovuta mashabiki ilikuwa ni ile kati ya AS Monaco na PSG.
Mchezo huo ulimalizika kwa suhulu ambayo iliifaidisha vilivyo Monaco ambayo ilifanikiwa kufikisha pointi 42 na kuzidi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao.
Yalikuwa matokeo mazuri kwa Monaco lakini sio kwa PSG kwa sababu hiyo ililiwa ni sare yapili mfululizo kwenye ligi hiyo.
Ni kama timu hii inajidanganya kuhusu supastaa Kylian Mbappe, ambaye inajaribu kumuonyesha kwamba PSG ni kubwa na inaweza kuishi bila yeye.
Katika mechi nne zilizopita Mbappe amecheza tatu tu ambapo mbili alianzia benchi na moja alicheza kipindi cha kwanza na akatolewa kipindi chapili kiliporejea.
Mechi mbili za hivi karibuni kuanzia kwa Rennes na Monaco ambapo Mbappe hakumaliza dakika zote 90.
Kukaa benchi kwa Mbappe kumekuwa kukihusishwa na kile kinachoendelea baina yake na mabosi wa PSG ambapo amewakatalia kusaini mkataba mpya na kuendelea kusalia kwenye timu hiyo na badala yake anataka kuondoka mwisho wa msimu ambapo atakuwa mchezaji huru.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Ufaransa ni kwamba PSG inataka kumuonyesha Mbappe kwamba inaweza ikacheza bila ya kumtegemea yeye na bado ikapata matokeo. Lakini hilo linaonekana kuwa gumu kwa sababu hajaonekana bado mtu wa kuziba pengo lake.
Hatari iliyopo kwa PSG ni kwamba ikiendelea kuangusha pointi kuna uwezekano Brest ambayo ipo nyuma yake ikaishusha kileleni na stori ikabadilika.
Msimu huu staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa amefunga mabao 21 kwenye mechi 22 za Ligue 1. Ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye kikosi cha PSG na Ligi Kuu Ufaransa.