Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

PSG? Sio kweli

Mo Salah 2 Mohammed Salah

Sat, 17 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

PRESHA imewapanda mashabiki wa Liverpool, wakiwaza itakuwaje msimu ujao? Msimu uliopita mambo hayakuwa matamu, wamekwama kwenye mpango wao wa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Sasa itakuwaje kama wakimpoteza staa wao makini kabisa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na mambo yatakavyokuwa kwenye Ligi Kuu England msimu ujao?

Presha kwa mashabiki wa Anfield. Lakini, wakala wa staa huyo, ambaye ni Mohamed Salah – ameshusha watu presha baada ya kuwaambia, mteja wake si kweli kwamba amekutana na mabosi wa Paris Saint-Germain kwa ajili ya kwenda kukipiga kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ufaransa msimu ujao.

Liverpool imeshawapoteza mastaa wake muhimu wa kikosi cha kwanza kwenye dirisha hili wakiwamo Roberto Firmino, James Milner na Alex Oxlade-Chamberlain – hivyo kumpoteza na Mo Salah si kitu kitakachochukuliwa kimzaha.

Mashabiki wa Liverpool wana hofu kubwa kwa sababu kama Mo Salah akiondoka basi hawatakuwa na nguvu kubwa ya kuchuana na Manchester City kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na mataji mengine msimu ujao.

Juzi Alhamisi kuliibuka ripoti kwamba Mo Salah amekutana na rais wa klabu ya PSG, Nasser Al-Khelaifi.

Al-Khelaifi anaripotiwa kuingia mzigoni kufanya usajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na alifanya mpango wa kunasa saini ya Mo Salah. Imeripotiwa bosi huyo amekuwa akiwasiliana na Mo Salah tangu kipindi ch mapumziko ya Kombe la Dunia na kwamba wiki iliyomalizika kulikuwa na kikao kwa kuwa anamtazama mkali huyo wa kimataifa wa Misri kuwa mtu sahihi wa kwenda kurithi buti za Lionel Messi huko Paris.

Lakini, wakala wa Mo Salah kuweka sawa mambao aliibuka na kudai hakuna mkutano wala mazungumzo ya aina hiyo yaliyofanyika, hivyo hakuna uhamisho utakaomhusu Salah.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, wakala Ramy Abbas Issa aliandika: "Hapana, hakukutana na mtu. Kufupisha stori."

Salah hakufurahishwa na namna Liverpool ilimaliza msimu wa 2022-23 na hakuficha hilo baada ya kuliweka wazi. Alikuwa mchezaji wa kwanza wa Liverpool kuwatumia ujumbe mashabiki baada ya mechi ya mwisho ya msimu.

Akiwa kwenye picha ya rangi nyeusi na nyeupe, Mo Salah aliandika kwenye Twitter: "Nimehuzunika sana. Hakuna kutoa kisingizio kwenye hili. Tulikuwa na kila kitu tulichohitaji ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na tumeshindwa.

"Sisi ni Liverpool na kufuzu michuano hiyo ni jambo muhimu. Naomba radhi, lakini hii kitu inavunja moyo sana. Tumewaangusha na tumejiangusha pia."

Kwa upande wake, kocha Jurgen Klopp anamtarajia Mo Salah kubaki Anfield na kuisaidia Liverpool kupona kwenye vidonda vya kuboronga msimu uliopita. Kabla ya mechi ya mwisho ya kufunga msimu, kocha huyo Mjerumani alisema Salah ataendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi chake.

"Sina wasiwasi, la. Nimesikia vingi sana vinavyosemwa, lakini siwezi kusema kitu chenye mwelekeo huo. Kwa kifupi tu Mo Salah anapenda kuwa hapa na atakuwa sehemu ya mipango. Ameomba radhi kwa kile tulichofanya,” alisema Klopp.

"Kama kutakuwa na mchezaji atakuja na kusema, 'oh, hatukufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, naondoka', Nitamwendeesha mwenyewe hadi kwenye klabu anayotaka kwenda. Nitachukua funguo na kumwambia 'njoo kwenye gari, unataka kwenda wapi, nitakuendeesha'.

"Hilo haliwezi kuwa tatizo la Mo na hakuna mchezaji aliyesema hivyo, Ni hivyo."

Chanzo: Mwanaspoti