Nani aliyekuambia kucheza soka hupoteza mvuto kwa mtoto wa kike? Straika mkali na fundi wa mpira, Philomena Daniel, licha ya kucheza kwa kiwango cha juu, lakini bado ile haiba yake ya kike na urembo haujamtoka kiasi ni ngumu ukikutana naye kitaani na kuambiwa ni mwanasoka.
Ni rahisi kumtambua Philomena akiwa uwanjani, lakini akiwa mtaani ni ngumu kwani ulimbwende unamfanya aonekane kama mwanamitindo flani, tofauti na zile pilikapilika zake za kutaka kuwaliza makipa wa timu pinzani katika Ligi Kuu ya Wanawake (TWPL).
Mwanaspoti limefanya mahojiano na staa huyo anayekipiga Yanga Princess iliyomsajili msimu huu kutokea Mlanzidi Queens na kufunguka mambo mengi, ikiwamo ishu ya kushindwa kucheza muda mrefu kutokana na kuumwa kila aingiapo uwanjani. Tiririka naye...!
KWA NINI SOKA
Philomena anasema soka ni kazi aliyoichagua na ipo ndani ya damu kiasi kwamba anakuwa tayari kuhimili changamoto, lakini ingekuwa ya kuchaguliwa na mtu angekata tamaa.
“Mpira ilitokea tu nikajikuta nauweza sijui hata ilikuwaje, lakini ndio uhalisia, Mungu akiamua kukuchagulia nini cha kufanya huwezi kupingana naye,” anasema.
Philomena anasema japo ilikuwa ngumu mama’ke kukubali alipomwambia anataka kucheza soka, lakini alipambana kutetea ndoto akipigania kuonyesha kipaji kwa familia kuwa hajakosea njia maana ilikuwa haitaki.
KUSHINDWA KUCHEZA
Mchezaji huyo anasema tangu atue Yanga amekuwa na wakati mgumu kuitumikia kutokana na kuumwa kila uchao akishindwa kujua shida ni nini.
Anasema amekuwa akiumwa tu aingiapo uwanjani, hivyo hali hiyo kumfanya kuzidi kuwa mnyonge zaidi.
“Hata sijui kabisa shida nini jamani nashindwa kujua, nikiingia tu uwanjani naumwa yaani sijielewi elewi, ila namuomba Mungu anisaidie hii hali iishe,” anasema, huku kocha wake, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ akisema anamtegemea mchezaji huyo na ndio sababu ya kumsajili dirisha dogo, hivyo kuumwa kwake kumeikosesha timu vitu.
“Ni kweli amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti mara kwa mara, lakini anaendelea vizuri, Mungu mwema atapona, tunaumia kumkosa wakati anahitajika sana ndani ya timu.”
ELIMU CHALI
Kutokana na kipaji chake, Philomena aliamua kuishia kidato cha pili, huku muda mwingi anaeleza kuw aaliutumia kufanya bidii katika kipaji chake, akijituma mazoezini na kucheza kwa nidhamu.
Anasema pamoja na hilo, lakini kingine kilichomsukuma kukatisha masomo ni ukata uliokuwa kwenye familia, jambo lililochangia kupambana katika soka ili kumpunguzia mama yake majukumu aliyoyaona yapo ndani ya uwezo wake, huku akidokeza soka ilikatisha ndoto yake ya kuwa daktari.
Philomena anasema mama yake alikuwa kila kitu katika maisha baada ya baba mzazi kuikimbia familia, ambapo aliwapambania kuhakikisha wanakula na kusoma katika mazingira magumu.
“Nilivyoona mama anahangaika kututafutia ada mambo yanakuwa magumu nikaona isiwe shida kumchosha, kwani niliona alivyokuwa anakosa amani ama anapambana kwa jasho ili sisi tutimiziwe mahitaji muhimu, nikaona mpira utanitoa na nitamtunza.”
Anasema: “Lakini naumia kwamba mama yangu hakufaidi matunda ya kazi ambayo nilitamani nifanye kwa jasho - iwe jua ama mvua, amefariki miaka mitano nyuma, sitasahau, kuna wakati nikikumbuka nalia sana, ila kazi ya Mungu haina makosa.”
Mchezaji huyo anasema kwa kuwa baba yao aliwakimbia na baada ya mama kufariki, aliona wamebaki yatima wanaotakiwa kujipambanua nini wafanye ili maisha yaende kiuchumi.
“Hakuna kitu ambacho kiliniumiza maisha yangu kama kifo cha mama, halafu bahati mbaya sikuweza hata kumuona nilikuwa sipo nyumbani nikakuta makaburi tu washazika,” anasema.
CHANGAMOTO
Philomena anasema changamoto ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, ila upande wake anasema anakumbana na wakati mgumu toka alipotua Yanga Princess dirisha dogo.
“Mimi ni mshambuliaji ndiyo nafasi ninayoimudu sana, lakini toka nimesajiliwa Yanga nimekuwa na wakati mgumu sana wa kuumwa mara kwa mara hata ninachoumwa sikijui.
“Inaweza kuwa siku ya mechi niko vizuri, lakini ukifika muda tu naingia uwanjani miguu inaishiwa nguvu nakuwepo kuwepo tu sijui ni nini, inaniumiza sana hii hali namuomba sana Mungu,” anasisitiza mchezaji huyo anayemzimia beki Shomary Kapombe wa Simba.
“Namzimia sana Kapombe, namkubali ni beki lakini muda mwingine anacheza kama ‘mido’ anajua sana na anatoa msaada mkubwa kwa timu ya Simba na hata ya Taifa.
“Wapo wachezaji wengi ila Kapombe ni mtu sana, kuna siku nikionana naye nitapata vitu vingi kutoka kwake.”
Kwa upande wa wanawake, anasema anamkubali Asha Rashid ‘Mwalala’ kutokana na uwezo wake awapo katika majukumu.
“Hata kabla sijatoka kufika hapa nilipo, Mwalala ni mchezaji ambaye nilikuwa nikimtazama uwezo na majukumu yake awapo katika eneo lake.”
NJE YA SOKA
Straika huyo anasema mbali na soka, anapenda kusikiliza muziki na kutazama ‘movie’ zinazomfanya akili ichangamke zaidi.
“Hata nikimaliza majukumu ya uwanjani, napenda sana kupika na najua kupika vyakula vingi tu. Mbali ya kuwa mchezaji lakini pia ni mama mtarajiwa,” anasema mchezaji huyo aliyekuwa na ndoto za kuja kuwa daktari tangu akiwa utotoni, lakini kukosa kwake ada kulimkatisha na kujitosa kwenye soka anakokiri ndani ya Yanga kuna ushindani wa namba.
“Kama hapa Yanga ushindani ni mkubwa ambao unakufanya mchezaji uwaze namna gani utamfanya kocha akupe nafasi ya kucheza. Vita ya namba inazidi kwa kuwa kila mchezaji anatakiwa kuwa na uwezo wa kupambana, kocha ni mkali tunapokosea, hataki masihara, tofauti na Mlandizi.”
MCHUMBA WA MTU
Kama baadhi ya wasichana, Philomena ana mchumba ambaye ni mwanasoka anayetokea Zanzibar.
“Mchumba wangu yupo Zanzibar na tunapendana sana tu, Mungu akipenda kama ndiye mume basi itakuwa, maana mimi ni mwanamke wa kuwa na familia, ni jambo lisilopingika,” anasema huku akifichua lengo lake ni kucheza soka nje ya nchi akifuata nyayo za Mwanahamisi Omary aliyepo Morocco.
“Kila mchezaji anakuwa na malengo hayo, na Mwanahamisi keshaendelea, walishaifungua milango kina Mwasikili, hivyo hata sisi tutatoboa tu,” anasema Philomena aliyewahi kucheza timu ya taifa ya U20, japo kiu yake ni kuichezea Twiga Stars kwa kiwango cha hali ya juu.
“Timu ya wakubwa sio sana, sipati nafasi huko kama ilivyokuwa U-20 huku ndiko ninaitwa mara nyingi na namshukuru sana Kocha Shime kuniona na kunijumuisha na wenzangu.”
ALIKOTOKA
Philomena anasema alianza kusakata soka akiwa kwao Morogoro ambako alikuwa anaishi, baadaye akafanikiwa kutua Mlandizi Queens na sasa Yanga.
“Nilikuja Dar es Salaam aliniona Seba nikacheza timu ya Taifa ya vijana tulienda Nigeria, nilivyokuwa timu ya taifa ndio Mlandizi waliniona na kunisajili,” anasema.
Mchezaji huyo alidumu Mlandizi Queens miaka mitano na baada ya kung’ara dirisha dogo msimu huu Yanga wakamuona na kumpa kandarasi ya mwaka mmoja.
UGANDA, Alikiba
Philomena anaitaja mechi ambayo hataisahau kuwa ni ile ya 2019 alipoichezea timu ya taifa ya chini ya miaka 20 dhidi ya Uganda kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
“Najua wachezaji wengi hawataki kukubali kuambiwa wamecheza chini ya kiwango lakini hata kabla ya kuambiwa tayari nilikuwa nimejiona.
“Nje ya soka napenda sana muziki, hata wakati mwingine nikiwa mazoezini utanikuta nasikiliza muziki na Alikiba ndiye msanii ambaye sichoki kumsikiliza, maana nyimbo zake zina hisia kali na ujumbe mzito kwenye simu yangu nina nyimbo zake kama zote,” anasema.