Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

PAOK hili ndilo chama la Samatta

Samatta Mbwana Ally PAOK hili ndilo chama la Samatta

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Julai 17, 2023, miamba ya soka la Ugiriki, PAOK ilitangaza kumsaini nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwa mkataba wa miaka miwili huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Hii itakuwa klabu ya tano kwa Samatta kuichezea barani Ulaya, ikumbukwe kuwa safari yake ilianzia KRC Genk ya Ubelgiji ambako alijipatia umaarufu mkubwa hadi kuzivutia klabu mbalimbali za Ligi Kuu England na mwishowe akatua Aston Villa.

Mambo hayakwenda kama ambavyo ilikuwa ikitarajiwa nchini England licha ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kucheza ligi kuu nchini humo (EPL) akaibukia Uturuki baada ya kuwekwa sokono.

Ndani ya miaka mitatu kati ya minne ya mkataba wake na Fenerbahce, Samatta alijikuta akitoka mara mbili tofauti kwa mkopo, aliichezea Antwerp na kurejea tena Genk kabla ya kutua PAOK.

Mara baada ya kukamilisha uhamisho huo, Samatta alisema, "Habari PAOK. Nina furaha kuwa hapa… Siwezi kungoja kuwaona nyote na kuipigania klabu. Lakini naamini nitakuona hivi karibuni."

PAOK ni miongoni mwa timu kubwa na kongwe barani Ulaya yenye historia ya namna yake na haya ni mambo machache kuwahusu.

ILIPOASISIWA

PAOK FC timu ya soka inayotoka kwenye klabu ya michezo ya AC P.A.O.K. na ina uhusiano wa karibu na Hermes Sports Club iliyoanzishwa mwaka 1875 na jumuiya ya Kigiriki ya Pera iliyotoka Uturuki kwenye mji wa Constantinopo (Instanbul ya sasa).

Klabu hiyo ilianzishwa Aprili 1926 na wakimbizi kutoa Uturuki (Constantinopolitan/Instanbul) ambaye alikimbilia Ugiriki katika mji wa Thessaloniki baada ya kushindwa kwa Wagiriki katika Vita vya Greco-Turkish.

Sera ya PAOK ilikuwa wazi kwa kila raia wa Thesaloniki kushiriki soka na kusababisha kuanzishwa kwa timu nyingine ya AEK Thessaloniki na kuruhusu wakimbizi pekee kucheza.

Nembo asili ya PAOK ilikuwa kiatu cha farasi na karafuu yenye majani manne.

PAOK ilicheza mechi yao ya kwanza ya kirafiki Mei 4, 1926 kwenye uwanja wa Thermaikos na kuishinda Megas Alexandros Thessaloniki 2-1. Kocha wa kwanza wa klabu hiyo alikuwa Kostas Andreadis ambaye alitumia miaka mitano kwenye benchi la timu bila kudai malipo. Nahodha wao wa kwanza alikuwa Michalis Ventourelis.

MASHABIKI USIPIME

PAOK FC ndiyo klabu ya kandanda inayoungwa mkono zaidi na watu wengi Kaskazini mwa Ugiriki kulingana na kura na tafiti zilizofanywa.

Wafuasi wa kitamaduni wa PAOK wanatoka katika jiji la Thessaloniki, ambako klabu hiyo ina makao yake, pia kutoka eneo lote la Macedonia na Kaskazini mwa Ugiriki.

Pia wana mashabiki kote kwenye nchi hiyo na katika wazawa wa Ugiriki walio katika mataifa mengine ya Ujerumani, Australia, USA na kwengineko.

Utafiti uliofanywa na Marca mnamo Agosti 2018 uliripoti PAOK ndio timu maarufu ya soka ya Ugiriki kwenye mitandao ya kijamii.

WAPINZANI

Mahasimu wakubwa kwenye soka la Ugiriki ni Olympiacos na PAOK sawa na ushindani uliopo hapa nchini wa Simba na Yanga.

Upinzani huo uliibuka miaka ya 1960, Olympiacos ilipojaribu bila mafanikio kumpata nyota wa zamani wa aliyeng'ara akiwa na PAOK, Giorgos Koudas, hivyo kumsajili bila kuifuata PAOK kuzungumza nao.

Ushindani mkali na wa muda mrefu kwa PAOK upo pia kwa timu za Aris FC, Panathinaikos na AEK ambazo ni klabu mbili kubwa za Athens, mji mkuu wa Ugiriki.

MAFANIKIO

Ligi Kuu (Super Ligi)

Ubingwa (3): 1975–76, 1984–85, 2018–19

Kombe la Ugiriki

Ubingwa (8): 1971–72, 1973–74, 2000–01, 2002–03, 2016–17, 2017–18, 2018–19, 2020–21

KOMBE LA WASHINDI (UEFA CUP WINNERS):

Robo fainali (1): 1973–74

EUROPA CONFERENCE LEAGUE

Robo fainali (1): 2021–22

MACEDONIA FCA CHAMPIONSHIP:

Ubingwa (7): 1936–37, 1947–48, 1949–50, 1953–54, 1954–55, 1955–56, 1956–57

MACEDONIA–THRACE FCA CHAMPIONSHIP:

Ubingwa (1): 1939–40

Chanzo: Mwanaspoti