Matajiri wa soka nchini, Azam FC imepoteza matumaini yua kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini mabosi wa klabu hiyo wameanza mipango ya kuisuka timu kwa msimu ujao ikipanda kuleta majembe ya maana akiwamo Ousmane Ouattara.
Nyota huyo wa Ivory Coast anayekipiga klabu ya US Monastir ya Tunisia akiwa ni mmoja wa mabeki wa kati wa timu ya taifa ya nchi yake, tayari ameanza mazungumza na mabosi wa Azam ili atue kikosini kwa msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya Azam, zinasema kuwa mabosi hao wamepanga kuboresha kikosi hicho katika maeneo kadha ikiwamo la kipa, ikielezwa huenda ikaachana na mmoja kati ya watatu walionao kwa sasa, ili kumleta kipa wa Enyimba John Noble Barinyima.
Makipa wa sasa wa timu hiyo, Mathias Kigonya, Ahmed Selula na Wilbol Maseke wameshindwa kuonyesha viwango bora kwenye michezo mingi ya Ligi Kuu na hata ile ya ASFC, huku ikielezwa hata benchi la ufundi nalo huenda likakumbwa na fagiafagia hiyo.
Michakato hiyo ya usajili kwa Azam inaendelea kimya kimya ili kuepuka presha ya kufanya hivyo wakati wa dirisha usajili kutokana na timu nyingi huenda zikawania saini za wachezaji zinaowahitaji na chanzo cha kuaminika ndani ya klabu hiyo imesema matokeo iliyoyapata katika ligi kwa msimu huu yamewatibua wengi tofauti na malengo.
Hakuna kiongozi wa Azam aliyekuwa tayari kuzungumza kwa kina taarifa hizo za usajili kwani simu zao zilikuwa zikiita tu, bila kupokelewa na timu hiyo kesho itakuwa wenyeji wa KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.