Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ouma hana deni kwa Wagosi

Ouma Coasta.jpeg Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma

Sun, 26 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuiwezesha Coastal Union kukata tiketi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao kwa kushika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu Bara, kocha wa timu hiyo, David Ouma amesema asidaiwe chochote kwa sasa kwani alishatimiza malengo aliyoelekezwa mara tu alipotua nchini kuinoa timu hiyo.

Kocha huyo raia wa Kenya aliingia mkataba wa miaka miwili kuiona timu hiyo akichukia mikoba ya Mwinyi Zahera na alipewa malengo ya klabu msimu huu ya kushika nafasi nne za juu ambayo yaliendana na falsafa yake.

Mafanikio ya Wagosi hao huenda yakawaneemesha kwenye dili za udhamini kwani waliahidiwa na mdhamini wao wa jezi Elsewedy Cables ikimaliza ya nne na kukata tiketi ya CAF itaongeza udhamini ikiwemo kuipeleka timu Misri kujiandaa na msimu mpya.

Coastal ilijihakikishia nafasi hiyo baada ya kuvuna alama moja nyumbani dhidi ya JKT Tanzaniana kufikisha pointi 42 ambazo haziwezi kufikiwa na timu zilizopo nyuma yao.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha Ouma amesema kwa alichokifanya hana deni na Wagosi kwa sasa na anajivunia wachezaji, makocha wenzake, viongozi na wadau wote wa klabu hiyo na sasa ni kuanza maandalizi mapema kwa msimu mpya ili nafasi waliyoipata waitumie vyema.

"Wakati ninakabidhiwa timu niliambiwa malengo ya msimu huu ni kushika nafasi ya nne katika ligi, nami kwa falsafa yangu nimeiinua timu kutoka chini hadi kufikia lengo, japo niliiwazia sana nafasi tatu za juu, ila kila kitu huwa na mwanzo wake," alisema Ouma na kuongeza;

"Haikuwa rahisi kufikisha timu hapa ilipo msimu huu. Ligi ya Tanzania ni ngumu mno, kila timu unahitaji matokeo wachezaji wana ari kubwa ila mbinu ambazo tumezitumia wachezaji wetu wameweza kuzitumia vizuri."

Wakati Ouma akijinasibu kufikia malengo ya klabu, mashabiki na wapenzi wa Coastal wakiwemo Mohammed Abubakar na Amina Jumbe wamewapongeza wachezaji na benchi la ufundi, huku wakiuomba uongozi kufanya usajili wa wachezaji ambao wataifanya timu kufanya vizuri kitaifa na kimataifa msimu ujao.

"Malengo yakishatimia huwa ni furaha kwetu mashabiki, sasa tunauomba uongozi ufikirie makubwa zaidi, waboreshe benchi la ufundi pamoja na usajili wa wachezaji ufanyike ule wa maana kulingana na mahitaji ya kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao, timu itakuwa na mechi nyingi zaidi," alisema Abubakar.

Wagosi iliyowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 1988 (wakati ikiwa Ligi Daraja la Kwanza) na kushiriki Kombe la Washindi 1989 ikiwa ni mara ya mwisho kwa timu hiyo kucheza michuano ya CAF, imesaliwa na mechi moja itakayopigwa kesho Jumanne dhidi ya KMC iliyotoka kufungwa bao 1-0 na Simba.

Chanzo: Mwanaspoti